Patanisho: Mwanadada atoka kimapenzi na mume wa dadake baada ya kuhamia kwao ili kumsaidia

Hellen alikiri kuwa mume wa dadake alikuwa amefanya majaribio kadhaa ya kumtongoza lakini akakataa.

Muhtasari

•Hellen alifichua kwamba ugomvi kati yake na Selina ulitimbuka takriban miaka miwili iliyopita baada ya dada huyo wake mkubwa kuanza kushuku kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mume wake.

•Hellen alikata simu punde baada ya kuagizwa aseme ukweli.

Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi, kitengo cha Patanisho, mwanadada mmoja aliyejitambulisha kama Hellen Halima (20)  alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na dada yake Selina Ann (26).

Hellen alifichua kwamba ugomvi kati yake na Selina ulitimbuka takriban miaka miwili iliyopita baada ya dada huyo wake mkubwa kuanza kushuku kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mume wake.

"Ilikuwa 2020. Nilikuwa nimeenda kwake baada ya kujifungua mtoto. Nilienda kukaa naye nikamshughulikia mpaka akapata nguvu. Baadae nilipata kazi mahali ambapo mumee alikuwa anafanya kazi. Dadangu alianza kushuku kuwa niko na mume wake kwa sababu yeye ndiye alinitafutia kazi," alisimulia.

Hellen alidai kuwa dada yake alimtimua kutoka kwake usiku baada ya kumhusisha kimapenzi na mumewe.

"Nilienda nikatafuta nyumba kwingine kwa sababu nilikuwa na pesa. Asubuhi ilipofika alikuja akachukua kila kitu nilichokuwa nacho, hatukuongea tena. Baadae alinipigia simu na kunitusi," alisema.

Alipuuzilia mbali madai ya kutoka kimapenzi na mume wa dadake na kudai kuwa mkubwa huyo wake alikuwa anasikiliza sana fitina za watu na kuziamini. 

Hata hivyo alikiri kuwa mume wa Selina alikuwa amefanya majaribio kadhaa ya kumtongoza lakini akakataa.

"Hatujawahi kuongea na mzee kwa sababu bibi yake atanitusi," alisema.

Selina alipopigiwa simu alimwagiza dadake kusema ukweli kuhusu yote  yaliyotokea kati yake na mumewe. Alidai kwamba ana uhakika dadake alikuwa akitoka kimapenzi na mumewe na kusema jambo hilo limemuathiri sana kisaikolojia.

"Hiyo stress karibu inaniua. Sijui mbona ananitafuta na hata alikana kuwa yeye si dada yangu," alisema.

"Siwezi kukusamehe saa hii. Nitakusamehe baadae. Kwanza useme ukweli. Ukisema ukweli mlikuwa mnalala naye nitakusamehe," Selina alimwambia dadake.

Hellen alikata simu punde baada ya kuagizwa aseme ukweli.

Selina alisema, "Alitafuta nyumba alafu akaanza kuwa na kiburi. Mume wangu alianza kupatana na yeye usiku.  Baadae nilikuja kuwapata red handed kwa nyumba. Mume wangu alikuwa akisema ati anaenda kazi ya usiku."

Alibainisha kuwa itakuwa ngumu kukubali kumsamehe dada yake kwani yaliyotokea yalimuumiza sana.

Hata hivyo alisema alimsamehe mumewe baada ya tukio hilo na wamekuwa wakiishi pamoja.