"Simjui, sio mume wangu, sijui kama niko na mimba yake!" Mwanadada amkana mumewe waziwazi

Mercy alipopigiwa simu, alijibu kwa ukali na hata kudai kwamba hamfahamu Michael.

Muhtasari

•Michael alisema mkewe alitoroka ndoa yao ya miaka miwili akiwa mjamzito baada ya kukosa kutimiza ombi lake la kununuliwa simu.

•Mercy hata hivyo aliendelea kumkana jamaa huyo na hata akamshauri atafute mwanamke mwingine wa kuoa.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, Michael Wekesa ,35, kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake  Mercy Nasimiyu ,23, ambaye alikosana naye mwezi Machi kufuatia mzozo wa simu.

Michael alisema mkewe alitoroka ndoa yao ya miaka miwili akiwa mjamzito baada ya kukosa kutimiza ombi lake la kununuliwa simu.

"Ilifika wakati akasema nimnunulie smartphone kama yangu.Nilimwambia angoje kidogo nipate pesa nitamnunulia. Akauliza kwa nini najinunulia na siwezi kumnunulia. Alikasirika akasema ni kama simpendi. Kidogo kidogo akatoroka akaenda kwao," alisema Michael.

Alisema Mercy amekataa katakata kurudiana naye licha ya kumfuatilia.

"Mahari sijatoa. Kwao nilienda wakati nilimuoa," alisema.

Mercy alipopigiwa simu, alijibu kwa ukali na hata kudai kwamba hamfahamu Michael.

"Wewe achana tu na mimi na ukae," Mercy alimwambia Michael.

Alisema, "Sikumwambia aninunulie simu. Siongei na yeye. Amekudanganya. Ata simjui. Mimi sijui chenye alinifanyia. Mimi sijui kama niko na mimba yake. Mimi sio mke wake. Mimi simjui Wekesa."

Licha ya Mercy kukana, Michael alisisitiza kwamba mpenzi huyo wake ni mjamzito na akafichua kwamba ana mtoto mwingine mmoja.

"Wakati ule sikuwa na pesa ya kukunulia simu. Pesa ikipatikana nitakununulia simu. Kama nimekosea kwa namna nyingine naomba msamaha," Michael alimwambia Mercy.

Mercy hata hivyo aliendelea kumkana jamaa huyo na hata akamshauri atafute mwanamke mwingine wa kuoa.

Michael alijibu, "Mimi sina wakati wa kuoa. Nilikuwa namsubiri yeye. Nilikuwa nimesema nitangoja hii mwaka iishe alafu mwaka ujao katikati nitafikiria kutafuta mwingine."