Aliyekuwa msanii wa lebo ya Sol Generation, Crystal Asige ameweka wazi kuwa sasa hana tatizo lolote na mabosi wake wa zamani, Sauti Sol.
Katika mahojiano na mtangazaji Massawe Japanni kwenye Redio Jambo, mwimbaji huyo hata hivyo alifichua kuwa hajazungumza na wanabendi wote wanne wa kundi la Sauti Sol kwa muda mrefu.
Alisema licha ya mzozo wake na bendi hiyo ya wasanii wanne katika siku za nyuma, hana vita yoyote naokwa sasa.
"Niko sawa najamaa hao, sina shida na wao," Crystal alisema.
Seneta huyo maalum alibainisha kwamba alikuwa akipigania tu haki yake wakati alipowashtaki mabosi hao wake wa zamani.
“Sijazungumza nao kwa muda mrefu. Lakini mimi najua hakuna kitu kama hicho. Ni kwamba nilitaka tu haki yangu,” alisema.
Huku akifunguka kuhusu mzozo wake na Sauti Sol ulipoanzia, mwimbaji huyo mwenye sauti ya kumtoa nyoka pangoni alisema, “Waliniomba niondoke kwenye lebo, hawakuona ushirikiano wetu ukiendelea, nikasema ni sawa.”
Mwaka jana, Crystal Asige ambaye aliteuliwa kuwa seneti baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2022 kuwakilisha watu wanaoishi na ulemavu, aliishtaki bendi ya Sauti Sol akitaka mahakama iwalazimu kufichua ni kiasi gani cha pesa wamepokea kutokana na nyimbo alizochangia zikiwemo;, Lenga, Extravaganza, Ukiwa Mbali. , Intro na Favourite Song tangu mwaka wa 2019.
Kulingana na karatasi za mahakama, pia alitaka Sauti Sol waamriwe kumlipa fidia akitaka wapeleke taarifa zote za leseni kuhusu nyimbo alizolalamikiwa.
Crystal Asige alikuwa amewashtaki Sol Generation Records Limited, Bien-Aime Baraza, Polycarp Otieno, Willis Chimano, Delvin Mudigi na KLM Royal Dutch Airlines Kenya.
“Akiwa chini ya studio ya mshtakiwa wa kwanza (Sol Generation) mlalamikaji alitunga na kutumbuiza kwenye nyimbo maarufu za 'Extravangaza' na 'Ukiwa Mbali' pamoja na mshitakiwa wa pili na wa tano, na wenzake wakati huo wakijulikana kwa jina la Bensoul, Nviiri The Story Teller na kikundi cha Kaskazini mwaka wa 2019 na mchango wake ulithibitishwa kuwa hivyo,” ilisoma sehemu ya hati za mahakama za Crystal Asige.
Mwimbaji huyo mwenye sauti nyororo alisema usimamizi wa lebo hiyo kimsingi ulimfukuza mnamo Novemba 2019, miezi tu baada ya kusainiwa.