Virusi vya corona: Jinsi damu yenye rangi ya buluu kutoka kwa Kaa inavyotumika kukabiliana na corona

Kaa ana macho kumi, amekuwepo kwa takriban miaka milioni 300 na sisi hutumia damu yake ya buluu kuimarisha afya yetu.

Naam sio uongo ni sayansi ya jadi.

Kwa miongo kadhaa tumemuhitaji mnyama huyu wa baharini na damu yake kutengeneza dawa.

Na wakati huu wa Covid-19 dawa hiyo haijasahaulika, Wanasayansi wanamtumia mnyama huyu kuchunguza uwezekano wa kupata chanjo ya corona.

Kama zamani , wanamazingira walihoji jinsi utafiti wa matibabu unaathiri maisha ya kaa na kutaka wasitolewe damu.

Je wanyama hawa wanatusaidia vipi?

Wanyama hawa wa zamani ni muhimu kwa sababu damu yao ya buluu huwasaidia wanasayansi kuhakikisha hakuna viini hatari vya bakteria katika dawa mpya zinazotenegenzwa , bakteria ambao wanaweza hata kuua.

Kiwango kidogo cha damu hiyo huviua viini hatari na wanasayansi huitumia kuchunguza iwapo dawa mpya ziko salama. Na ni damu ya kaa hao ambayo sisi wanadamu tumefanikiwa kuipata ili kuweza kufanya hivyo.

Kila mwaka, maelfu ya kaa hukamatwa na kupelekwa katika maabara nchini Marekani ambapo damu yao hutolewa katika mishipa ya damu iliopo karibu na moyo wao.

Baadaye huachiliwa na kurudi katika asilia yao.

Hakuna anayejua athari yake.

Awali , wataalam walidhani kwamba kaa wote waliishi baada ya kutolewa damu hiyo.

lakini katika miaka ya hivi karibuni, inakadiriwa kwamba hadi asilimia 30 hufa baada ya shughuli hiyo.

''Sasa huchukua damu kutoka takriban kaa nusu milioni'', anasema Dkt Barbara Brummer, ambaye anasimamia kundi linalofanya kazi uhifadhi wa asilia katika jimbo la New Jersy, ambapo kaa wengi hupatikana nchini Marekani.

Katika mahojiano na BBC, anasema kwamba hakuna anayejua athari ambayo ukusanyaji wa damu hiyo hutoa kwa maisha ya kaa hao wakati wanaporudishwa katika maeneo wanayotoka.

Lakini baadhi ya makampuni makubwa yanayotengeneza dawa hutoa mfano wa takwimu ambazo zinasema kwamba idadi ya wanyama hao imesalia kuwa sawa kwa miaka michache baadaye.

Chanzo kingine?

Kwa miaka kadhaa, utafiti umefanywa kutengeneza kitu ambacho kinaweza kuchukua mahala pa damu hiyo ya buluu kutoka kwa kaa hao.

Na mwaka 2016...Wanasayansi walipata wazo mbadala ambalo lilikubaliwa kutumika barani Ulaya. Baadhi ya makampuni ya kutengeneza dawa nchini Marekani pia yalijiunga.

Hivyo basi tunauliza ni kwa nini tunalizungumzia suala hili hivi sasa?

Kwa sababu mwezi uliopita , shirika linaloamua ni nini kinachotengeza dawa kuwa salama nchini Marekani lilisema wazo hilo mbadala haliwezi kuaminika kufanya kazi vyema.

Kampuni ambazo zinataka kuuza dawa nchini Marekani zimeambiwa kuendelea kutumia damu ya kaa ili kuzipima dawa zao.

Hiyo ina maana kwamba kampuni yoyote ambayo ina chanjo ya virusi vya corona itahitajika kuithibitisha kwa njia ya zamani kwa kutumia damu ya kaa, iwapo inataka kuwauzia mamilioni ya raia wa Marekani.

Dkt. Brummer anasema kwamba anchunguza tena njia hiyo mbadala kwa sababu inatumika katika mataifa mengine. ''lengo ni kuacha kutegemea kaa hao'', anasema.

Kampuni ya Uswizi Lorza ilianza kutafuta chanjo mwezi uliopita - ambayo itafanyiwa majaribio miongoni mwa wanadamu - na hiyo haitahitaji damu ya buluu ya kaa hao, aliliambia jarida la wanyama .

Brummer anasema kuna takriban kampuni 30 zinazoifanyia kazi chanjo hiyo na kila kampuni lazima ifanye vipimo hivyo.

''Hivyobasi hofu yangu ni idadi ya kaa hao , kwasababu ni kiungo muhimu cha mazingira yetu''.