Wabunge kukutana kupitia mtandao ili kudhibiti maambukizi ya Covid-19

Kuanzia wiki hii maseneta watakuwa wakifanya mikutano ya kamati kupitia mtandao kwa lengo la kudhibiti maambukizi ya Covid 19. Spika wa bunge la seneti Kenneth Lusaka anasema mikutano kwenye bunge imesitishwa kwa mwezi mmoja huku ikihofiwa huenda maseneta zaidi na wafanyikazi wa bunge wakaambukizwa virusi hivyo.

Anasema hali hiyo huenda ikibadilika baada ya mwezi mmoja ambapo kamati muhimu zaidi huenda zikaruhusiwa kufanya mikutano bungeni kulingana na suala linalojadiliwa.

iIfuatayo ni mkusanyiko wa habari humu nchini;

Wizara ya afya imeweka mikakati kabambe katika Nyanja za ndege ili kuwahakikishia wasafiri na wafanyikazi usalama wao baada ya Kenya kufungua anga zake jana kwa safari za ndege za kimataifa.

Polisi katika kaunti ya Kisii wanamsaka mwalimu mkuu mmoja anayedaiwa kumbaka msichana wa miaka 15 na kutoweka baada ya msichana huyo kumfichua. Kamanda wa polisi wa eneo hilo Jebel Munene anasema wameanzisha uchunguzi wa kisa hicho.

Hakikisheni mmekubaliana majukumu yenu yakiwemo ya kifedha, wewe na mpenzi wako kabla ya kufunga ndoa. Mshauri Kadzo Ndhundhi anasema kuingia katika ndoa na mtazamo kuwa pesa zako, ni zako kibinafsi,  kisha za mchumba wako ni zenu pamoja huenda kukampelekea mwenzi wako kukosa imani nawe kuhusu masuala ya kifedha.

Muungano wa wauguzi nchini sasa unaitaka serikali kuwafidia wahudumu wote wa afya katika kaunti ya Kisumu watakaopatikana na virusi vya Corona baada ya kutumia barakoa duni kwa muda wa wiki tatu. Naibu katibu mkuu wa muungano wao Maurice Opetu anasema DCI na EACC wanastahili kuchunguza na kuhakikisha watengezaji na wasambazaji wa bidhaa hizo pamoja na  maafisa wa kaunti wanawajibishwa kwa utepetevu wao.

Tume ya uwiano na utangamano imeibua wasiwasi kuhusu ongezeko la matamshi ya chuki na uchochezi kwenye mitandao ya kijamii katika kauntii za Mandera na Marsabit. Mwenyekiti wa tume hiyo Simon Kobia anasema wanafuatilia majukwaa yote ya mitandao ya kijamii na watakaopatikana wakieneza matamshi ya chuki watachukuliwa hatua za kisheria.