Wabunge kuondoa wadhifa wa mwakilishi wa kike

Kivumbi kinanukia mbungeni baina ya wabunge wa kike na wenzao wa kiume kuhusiana na pendekezo la kuondolewa kwa nyadhifa 47 za wakilishi wa wanawake.

Tangu ianzishwe kuambatana na katiba ya mwaka 2010 kupiga jeki idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi wadhifa huo umekabiliwa na utata kila mara. Wanaokosoa wadhifa huo na ambao wengi wao ni wanaume wanasema hauna manufaa yoyote na kwamba unaongezea tu gharama mtoa ushuru.

Gazeti la The Star limebaini kwamba kamati ya bunge ya utekelezwaji wa katiba inapanga kuwasilisha kipengele katika katiba kufutilia mbali wadhifa huo.  Hata hivyo, pendekezo hilo limeibua hisia kali kutoka kwa viongozi wa kike ambao wameapa kulipinga bungeni.

Pendekezo hilo linajiri miezi mitano tu baada ya wabunge wa kiume kuungana kusambaratisha mswada wa kuongeza idadi ya wanawake bungeni. Mswada wa jinsia wa thuluthi tatu umeangushwa bungeni mara nne, mara nyingi zaidi kuliko mswada wowote ule. Katika kila jaribio hapakuwepo idadi ya kutosha ya wabunge 233 kuupitisha. Wengi wa wabunge wa kiume walisusia vikao hivyo.

Jeremiah Kioni ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya utekezwaji wa katiba, katika mahojiano ya kipekee aliambia gazeti la The Star kwamba hatua ya kupendekeza kuondolewa kwa wadhifa wa mwakilishi wa wanawake inatokana na swintofahamu iliyoko kuhusu muda unaohitajika kutekeleza sheria ya thuluthi mbili.

Kipengele hicho kilikuwa kimejumuishwa katika mapendekezo ya katiba ya Naivasha maarufu kama “Naivasha Accord” lakini kikaondolewa na kamati ya bunge. Katiba ya awali ilikuwa imependekeza kuwa wadhifa wa mwakilishi wa wanawake ungeondolewa baada ya miaka 20 kutoka siku ya kuanza kutekelezwa kwa katiba ya 2010.

Katiba ya sasa haieleza bayana kuhusu swala hili.