Wachezaji gwiji ambao mikataba yao inakaribia kutamatika

Huku msimu mpya wa kadanda ukikaribia kung'oa nanga, timu zimetia bidii kusajili wachezaji wapya, makocha wapya wameteuliwa na pia mikataba mpya zimetiwa sahihi.

Juhudi hizi zote ni za kuhakikisha kuwa timu hazijapoteza ma staa wao na pia kuwahakikishia kuwa klabu zao zahitaji huduma zao.

Kwa mfano, mshambulizi  wa Manchester United Marcus Rashford amesaini mkataba wa malipo ya £200,000 kwa wiki ili kusalia na kilabu hiyo hadi  Juni mwaka wa 2023, akiwa na chaguo la kuongeza muda huo kwa mwaka mmoja zaidi.

"Nitafanya kila niwezalo ili kuifanya kilabu hii kurejelea hadhi yake na kuipa mafanikio ambayo mashabiki wetu wanastahili" Alisema  Rashford baada ya kusaini mkataba mpya.

Hata hivyo, kuna wachezaji gwiji bara ulaya ambao mikataba yao inakaribia kutamatika huku wengi wakitarajiwa kuwa wakala wa bure (free agent) ifikiapo mwisho wa msimu ujao.

Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya wachezaji ambao watasalia kutafuta timu mpya ifikiapo mwisho wa msimu ujao.

Luka Modric

Bingwa huyu wa tuzo la mchezaji bora duniani al maarufu Ballon d'Or mwaka wa 2018, alikuwa na wakati mwema katika kombe la dunia la 2018 lakini hakuwa na msimu wa kufana na klabu yake Real Madrid.

Kiungo huyu wa kati anamezewa mate na vilabu vingi duniani na haijulikani kama Madrid watampea kandarasi mpya.

David De Gea

Kipa huyu wa Manchester United ni miongoni mwa wachezaji ambao bado wanaringa kuweka saini katika mkataba ambao klabu hiyo baada ya kuitisha pauni millioni 350 ambazo mashatani wekundu hawako tayari kulipa.

Christian Eriksen

Raiya huyu wa Denmark amemwacha kocha wake wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino na tumbo joto baada ya kukata kuongeza mkataba wake ndani ya White Hart Lane.

Kulikuwa na habari kuwa Eriksen huenda akajiunga na klabu ya Real Madrid lakini kufikia sasa hakuna habari zozote kuhusu hali yake na ikisalia hivo, ataondoka Spurs kama wakala wa bure mwishoni mwa msimu mpya ujao.

Wachezaji wengine ambao wamejipata katika hali ile ni Ilkay Gundogan wa Manchester City, Nabil Fekir wa Lyon, Timo Werner wa RB Leipzig na Edinson Cavani wa PSG.