Wahasiriwa wa maporomoko West Pokot wadai kutelekezwa, BBI ikipewa kapau mbele

West pokot-compressed
West pokot-compressed
Wakaazi wa kaunti ya West Pokot wameonyesha kutoridhishwa na jinsi serikali inavyojikokota kuwapa misaada ya kimsingi baada ya janga la maporomoko ya ardhi, Jumamosi.

Mkaazi Paul Limakau ameelezea masaibu wanayopitia bila huduma za kimsingi licha ya hali ya anga kuimarika, hawajapata misaada ya chakula.

"Hatujapata usaidizi wa serikali. Leo hii anga ni shwari na ndege za kijeshi zingekuja kuzipa familia zilizoathiriwa misaada ya dharura." alisema.

Aidha, wananchi hao walisema kwamba serikali imeangazia ripoti ya BBI zaidi na kuwatelekeza licha ya kwamba wao ndiyo waliowachagua viongozi katika nyadhifa tofauti serikalini.

Wakaazi hata hivyo, wamepongeza shirika la Kenya Red Cross kwa kujumuika nao huku wakitoa misaada ya dharura.

"Red Cross wamekuwa hapa tangu mkasa ulipotokea," alisema.

Mkaazi Reuben Teko alisema kwamba wanawake katika kambi ya Sebit hawajapata msaada wowote.

"Kuna mama mwenye mtoto wa umri wa siku tatu na hadi sasa hajapewa mavazi ya kujikinga kutokana na baridi kali. Ana blanketi moja tu. Nyumba yao ilisombwa na mafuriko," alisema.

Mnamo Jumatano asubuhi, Gavana John Lonyangapuo alipokea misaada ya chakula na pamoja na mahitaji mengine maalum kutoka wahisani ili kusaidia familia zilizoathirika.

Misaada hiyo ilitolewa Wakfu wa Al Khair, Kape matt, jamii ya wafanya biashara pamoja na makanisa na kusambazwa katika vijiji vya Mwino na Parua.

Kwa sasa, idadi ya waliofariki imetimia 58.

Lonyangapuo aliwasihi wahisani kutoa misaada zaidi kwa familia 10,000 zilizoachwa bila makao baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO