Wahudumu wa kliniki katika soko la Toi Kibra wawekwa kwenye karantini

mbagathi
mbagathi
Kliniki moja katika mitaa ya mabanda ya Kibra katika soko la Toi sasa kinaangaziwa na serikali baada ya wahudumu watano wa kliniki hiyo kumhudumia jamaa kutoka kaunti ya Bomet aliyefariki kutokana na virusi vya Corona.

Upo uwezekano mkubwa kuwa wahudumu hao walipokuwa wakimshughulikia jamaa huyo huenda hawakujikinga inavyotakikana na serikali hali ambayo imeifanya serikali kuanza kuweka mikakati ya haraka.

Takriban watu 24 wamewekwa kwenye karantini wakiwemo wahudumu hao wa kliniki wa Vostrum.

Ernest Kosgei wa miaka 55 alizikwa Alhamisi nyumbani kwake Kawaget, Bomet kaunti huku kifo chake sasa kikiipa seriakli kiwewe cha kuwatafuta watu ambao alitangamana nao kabla ya kufariki.

Matokeo ya maabara yalidhihirisha kuwa  Kosgei alifariki kutokana na corona.

Katibu msimamizi katika wizara ya afya Mercy Mwangangi alisema serikali imeanzisha mchakato wa kuwatafuta watu waliojumuika naye .

Kufikia sasa, seriakli imekuwa ikiangazia safari za jamaa huyo za mwisho katika mitaa ya Kibra, japo alikuwa anaishi peke yake katika mitaa hiyo ya Kibra, huenda alikuwa ametangamana na watu wengi sana.

Nyumba yake na sehemu zilizoko karibu zimefukizwa dawa ya kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.