Watafika mbele ya kamati hiyo ya wanachama 11 kuanzia saa nne asubuhi. Kulingana na mwenyekiti wa kamati hiyo, seneta wa Kakamega Cleophas Malala, pande zote mbili zitaanza kikao chao leo kwa kutoa mawasilisho ya mwanzo.
Muda mfupi baadaye spika wa bunge la kaunti ya kirinyaga Anthony Gathumbi, mwenyewe au kupitia mwakilishi atawasilisha madai yote dhidi ya Waiguru. Kamati hiyo wiki jana ilimuagiza spika huyo kufika mbele yake na kutoa majina ya wawakilishi watatu wa kaunti watakaoandaman naye. Gathumbi pia alitakiwa kutoa nakala 20 zilizochapishwa za stakabadhi zizilizotegemewa katika hoja ya kumuondoa Waiguru afisini. Pia alitakiwa kutoa majina ya mashahidi.
Wawakilishi hao wa kaunti Juni tarehe 9 walijadili na kupitisha hoja ya kumuondoa Waiguru mamlakani wakimshtumu kwa kukiuka katiba na kutumia vibaya mamlaka ya afisi yake. Jumatano, gavana huyo na mawakili wake - Kamotho Waiganjo na Paul Nyamodi watakuwa kizimbani kukabiliana na madai dhidi ya mteja wao.