Wake wa Marais wa Afrika watoa wito wa kuongeza raslimali katika kukabiliana na ugonjwa wa saratani

Wake wa Marais wa Afrika watoa wito wa kuongeza raslimali katika kukabiliana na ugonjwa wa saratani

NIAMEY, Niger, 7 Julai 2019 (PSCU) – Mama wa Taifa Margaret Kenyatta jana jioni alijiunga na Wake wa Marais wengine wa Afrika katika kutoa wito wa kuongezwa kwa raslimali katika harakati za kukabiliana na  ugonjwa wa saratani katika bara hili.

Wito wa kuchukua hatua dhidi ya  ugonjwa wa saratani ulitolewa na Wake wa Marais kwenye mkutano uliofanyika jiji kuu la Niamey, huko Niger,ambao ulichunguza njia za kushughulikia tatizo la ugonjwa huo barani Afrika.

Mama wa Taifa  yuko jijini Niamey kwa Kikao Kikuu cha 23 cha  Shirika la Maendeleo la Wake wa Marais barani Afrika, (OAFLAD) ambacho kitaanza leo.

Mama wa Taifa ambaye ni Makamu wa  Rais wa shirika  la OAFLAD anahudhuria kikao hicho kutokana na mwaaliko wa Dkt. Lalla Malika Issoufou ambaye ni Mkewe Rais wa Niger.

Harakati za kukabiliana na kushughulikia aina zote za saratani ni nyanja ambayo imemulikwa katika Mkakati wa pili wa shirika la Mama wa Taifa la Beyond Zero katika kipindi cha mwaka wa 2018 hadi 2022 ambapo  hatua za kushawishi uekezaji katika huduma zilizogatuliwa za kukabiliana na saratani ya matiti na ya mlango wa uzazi zimepewa kipau mbele ikiwemo tiba ya nasuri yaani fistula.

Kwenye taarifa ya pamoja iliyosomwa na Mkewe Rais wa Burkina Faso, Sika Bella Kaboré, Wake wa Marais waliazimia kushirikiana na washikadau wote kuunga mkono harakati za kukabiliana na  saratani.

“Sisi, Wake wa Marais wa Afrika, tungependa kutoa wito kwa jamii ya kimataifa, Muungano wa Afrika, mashirika ya kanda na maeneo, mashirika ya kijamii, serikali na washikadau wote kuunga mkono harakati hizi za kukabiliana na magonjwa yasiokuwa ya kuambukiza ikiwemo kuzuia na kutibu saratani,” kasema katika baadhi ya sehemu ya taarifa hiyo ya pamoja.

Mkutano huo kuhusu saratani huko jijini Niamey  uliofanyika pembezoni mwa  Kikao kikuu cha 12 kisichokuwa cha kawaida cha Viongozi wa Nchi na Serikali wanachama wa Muungano wa Afrika pia ulihutubiwa na Marais Mahamadou Issoufou wa Niger, Idriss Déby wa Chad na Roch Marc Christian Kaboré  wa Burkina Faso ambao waliahidi kujitolea kuunga mkono harakati za kukabiliana na ugonjwa huo ambao umekuwa chanzo cha maafa mengi barani Afrika.

Mapema, Mama wa Taifa alihudhuria mkutano wa kamati simamizi ya shirika la maendeleo la Wake wa Marais ambao ulijadili mapendekezo ya washauri wa kiufundi.

Mkutano huo wa kamati hiyo simamizi uliangazia ripoti ya makao makuu ya shirika la OAFLAD kuhusiana na yale yalioafikiwa katika kipindi cha kwanza cha nusu ya mwaka huu mbali na taarifa  ya hesabu za matumizi ya fedha kuanzia Mwezi Januari hadi Mei  mwaka huu.

Vile vile, kamati hiyo ilijadili kuhusu kikao kikuu kijacho kitakachozungumzia kuhusu migogoro ya kijinsia kwenye Mkutano wa saba wa viongozi wa Afrika na Japan kuhusu Maendelo  ya Afrika (TICAD7) utakaoandaliwa kwa ushirikiano na  Hazina ya Shirika la Umoja  wa Mataifa kuhusu Idadi ya watu (UNFPA) pamoja na kikoa kikuu kuhusu usawa wa kijinsi na kuwapa shime wanawake  kitakachofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utakaofanyika katika makao makuu ya Umoja huo huko mjini New York baadaye mwaka huu.