Wakenya 167 waliokwama India kurejeshwa nyumbani

Familia za wakenya 167 waliokuwa wamekwama nchini India sasa zina cha kuwapa tabasamu baada ya shirika la KQ kuratibu safari ya kuwarejesha nyumbani.

Maelezo hayo yametolewa huku wakenya wengine waliokwama Beirut ,Lebanon pia wakiishinikiza serikali kufanikisha kurejea kwao nyumbani .Serikali inatawaka wapate stakabadhi zifaazo kutoka kwa ubalozi mdogo nchini humo .

Balozi wa Kenya nchini India Willy Bett  amesema wengi wa waliokwama nchini India kwa ajili ya janga la corona walikuwa wamesafiri kupokea huduma za matibabu  ilhali wengine walikuwa watalii na baadhi yao walikuwa wanafunzi .

Hata hivyo watarejeshwa nyumbani kwa gharama yao  kwani ndege ya KQ inatarajiwa kuwarejesha  Nairobi Agosti tarehe 19  na watawasili Nairobi  saa  tatu kasorobo siku ifuatayo .

Nchini Lebanon ambako mlipuko katika mji mkuu Beirut ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 130 ,serikali ya kenya imethibitisha kwamba wakenya watatu walijeruhiwa katika tukio hilo .

Ms Halima Mohamud,  balozi wa Kenya  Kuwait  ambaye pia anasimamia Lebanon  amesema wakenya wote waliojeruhiwa wametibiwa  na kuruhusiwa kuondoka hospitalini .