Wakenya hawapaswi kufikiria Tanzania ni timu ovyo - Ghost Mulee

Kocha wa zamani wa Harambee stars Ghost Mulee anadai vijana wa Kenya walikua na uwoga kidogo katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Algeria katika kipute cha AFCON nchini Misri lakini wana uwezo wa kufanya vyema katika mechi ya pili dhidi ya Tanzania kesho na pia dhidi ya Senagal Jumatatu.

Stars walipoteza 2-0 katika mechi ya ufunguzi lakini bado wa uwezo wa kufuzu kwa awamu ya pili kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya.

Kulingana na mkufunzi huyo wa zamani wa timu ya taifa, alisema kuwa mechi hiyo ilikuwa na vipindi viwili tofauti kwani hakupendezwa na jinsi Harambee Stars walikuwa wanapoteza mipira mingi na pia mikakati yao ya kuzuia mpira sana.

Hata hivyo, Mulee bado anashikilia kuwa bao la kwanza lililofungwa kupitia mkwaju wa penati halikuwa halali kwani mlinzi Dennis Odhiambo hakumguza Youcef Atal.

Sikupendezwa sana na jinsi tulivyoshindwa kupeana pasi kila tulipopata mipira. Tulicheza mchezo wa kuzuia sana katika kipindi cha kwanza na pia hatukuwa tunajiamini kila tulipo pata mpira. Alisema Ghost Mulee.

Aliongeza,

Pia sina furaha kwani CAF wameamua kutumia teknolojia ya VAR kuanzia robo fainali kwani ukiangalia bao la kwanza, Dennis hakumguza mchezaji wa Algeria lakini sasa Kenya hawawezi lalamika.

Kenya sasa ina kibarua kigumu kwani itabidi wameshinda mechi yao dhidi ya Tanzania hapo kesho na kuomba kuwe na matokea mema katika mechi dhidi ya Senegal na Algeria.

Ingawa Mulee ana imani kuwa Kenya itawabwaga Tanzania, hata hivyo mtangazaji huyo aliwaonya wakenya ambao wanadhani kuwa Tanzania ni timu rahisi.

Wakenya wanadhani Tanzania ni timu tu nyingine, hapana. Nafikiria kuwa twafaa kuwa makini sana na pia hatujatemwa nje ya mashindano bado.

Kuna uwezekano kuwa Kenya itawabwaga Tanzania halafu mechi ya mwisho dhidi ya Senegal huku tukitarajia kuwa mechi yao na Algeria itazaa matokeo mema.

Naamini tukichapa Tanzania, wachezaji wetu watajikakamua dhidi ya Senegal kwani watajua kuwa watahitaji pointi moja ili wafuzu. 

Michuano hiyo ya Ubingwa bara Africa itaingia siku ya sita leo huku mechi tatu zikichezwa nchini Misri.

Viongozi wa kundi B Nigeria watacheza dhidi ya Guinea saa 5.30pm huku wakitafuta ushindi ili kufuzu kwa awamu ya pili. Mechi hio itafuatwa na mechi ya kundi A kati ya Uganda na Zimbabwe saa 8pm.

Waganda wanahitaji angalau sare ili kuwa na matumaini ya kufuzu huku Zimbabwe wakitafuta ushindi baada ya kupoteza dhidi ya Misri katika mechi ya ufunguzi.

&t=9s