Wakenya wachemka baada ya viongozi kuvunja sheria za covid-19

Wakenya Jumamosi, Mei 30, walichemka baada ya kuibuka kuwa walala hoi wanazidi kukandamizwa na serikali huku mabwenyenye wakisazwa.

Waliteta kuwa Wakenya wa kawaida wamekuwa wakikabiliwa vikali kuhusiana na sheria za coronavirus ilhali viongozi wanazikiuka bila kuchukuliwa hatua.

Picha za kundi la wanasiasa waliokongamana nyumbani kwa katibu wa muungano wa wafanyikazi Francis Atwoli ziliwasha moto mtandaoni.

Wabunge takribana 40 walikongamana na kufanya kikao na wanahabari kutangaza maafikiano yao. Hata hivyo, hawakuangazia maagizo ya wizara ya Afya kuhusu kuepuka mikusanyiko ya watu.

Wakenya walitaka kundi hilo la wabunge kupelekwa kwenye karantini ya lazima kama vile walala hoi wamekuwa wakifanyiwa. Wakenya wa kawaida wamekuwa wakitiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani wakidaiwa kutozingatia sheria hizo.

Aidha wapinzani wa kundi la Atwoli pia waliteta kwenye mtandao huku Seneta Kipchumba Murkomen akidai kuna uwezekano viongozi hao hata walipata kinywaji.

"Kama mnaweza kufungua baa fungueni kanisa pia. Tuwache ukora." alisema Murkomen.

Katika kaunti ya Nyandarua, Gavana Francis Kimemia pia alionekana na umati wa watu ambao hawakuwa wameangazia sheria za covid-19. Wengi walishangaa ni kwa nini viongozi wakuu wanapuuza sheria hizo badala ya kuongoza kama mfano mzuri.

Je sheria hizo zimewekwa kwa ajili ya mwananchi wa kawaida ama piaa hata viongozi ni swali ambalo wengi wanaulizana kila kuchao.