Walimu wakuu kupokonywa jukumu la kusimamia pesa za shule

Wizara ya Elimu inapanga kuwapokonya walimu wakuu wa shule jukumu la kusimamia pesa za shule zinazotolewa na serikali, gazeti la Star limeripoti.

Pendekezo hilo linatarajiwa kupokea upinzani mkali kutoka kwa walimu wakuu. Katika pendekezo hilo waziri wa elimu atapewa mamlaka kuteua maafisa wa kusimamia pesa za shule. Gazeti la the Star limepata nakala ya mapendekezo hayo.

Mwezi Machi alipokuwa akihojiwa waziri, George Magoha alitoa onyo kali kwa wafisadi katika sekta ya elimu akisema kwamba hali haitakuwa ya kawaida tena. Hii huenda ikawa hatua yake ya kwanza ili kuafikia onyo lake.

"Sitaruhurusu mtu yeyote kufuja raslimali za umma. Nitafanya kazi niliopewa na rais Uhuru Kenyatta kikamilivu,” Magoha aliambia kamati iliongozwa na spika Justin Muturi.

Kuna mapendekezo mawili, la kwanza waziri wa elimu anaweza kumteua mwalimu mkuu wa shule kusimamia maswala ya kifedha ya shule au kumteua mtu kutoka nje asiyekuwa mwalimu kusimamia raslimali na maswala ya kifedha ya shule.

Ikiwa pendekezo la pili litatumika, litaathiri sana mipango ya shule kwa sababu mipango ya kifedha ya shule imekuwa ikisimamiwa na walimu wakuu. Majukumu ya walimu wakuu katika kusimamia fedha yanajumuisha kutayarisha bajeti, uhasibu na kutathmini matumizi ya kifedha ya shule.