Wanafunzi 79 watakosa kufanya mitihani baada ya madai ya kutosajiliwa

Wanafunzi 79 wanaosomea udaktari katika chuo cha KMTC (Kenya Medical Training College) tawi la Kakamega huenda wakakosa kufanya mitihani yao kutokana na madai kuwa hawajalipa pesa ya kujisajili.

Wanafunzi hao wanasema kuwa walilipa shillingi 500 ya kujisajili mnamo mwaka wa 2016, na ni juzi tu walipigwa na butwaa baada ya kupokea habari kuwa hawatakalia mitihani yao ambayo inatarajiwa kuanza hivi leo.

Wanafunzi hao waliongeza kuwa walijaribu kutafuta suluhisho bila mafanikio manake wasipokuwa na nambari za usajili na nywila hawawezi fanya mtihani huo.

Mwalimu mkuu katika chuo hicho Jeremiah Ngomo alikiri kuwa kulikuwa na ucheleweshaji wa kuwasajili wanafunzi watakaokalia mtihani huo, akiongeza kuwa amezungumza na baraza la maofisa wa kliniki na wamekubaliana kuwa wataanza upya kusajili wanafunzi watakaofanya mtihani huo kwa muda wa wiki moja.