Wandani wa Rais Mustaafu Moi walitunukiwa ardhi ya umma

Maelezo mapya yalichipuka Jumanne vile jamaa wenye uhusiano wa karibu na familia ya rais Mutaafu Daniel Moi waliwagawia mamia ya ekari za ardhi wanasiasa wa Kanu waliokuwa na ushawishi mkubwa.

Wabunge waliambiwa kuwa Gideon Toroitich, mpwa wa rais Mustaafu Daniel Moi, pamoja na aliyekuwa waziri Simeon Nyachae waligawa shamba la shirika la Ustawi wa Kilimo ADC katika hali ya kutatanisha.

Ardhi hiyo hiyo inapatikana katika eneo bunge la Magarini Kaunti ya Kilifi.

Stakabadhi zilizowasilishwa kwa kamati ya bunge Jumanne inaonyesha kuwa Nyachae alikuwa miongoni mwa watu 125 na makampuni yalionufaika kwa kupewa ardhi hiyo.

Wakaazi wa eneo hilo wanadai umiliki wa ardhi hiyo, swala ambalo limevutia tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC).

Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa bungeni na Katibu wa utawala wa kilimo Andrew Tuimur, watu waliokuwa na ushawishi katika serikali ya Moi wanaongoza orodha ya waliogawiwa vipande vya ardhi katika shamba la ADC.

Waligawiwa shamba hilo badala ya wenyeji kupewa na ilhali wenyeji walikuwa wameachwa maskwota.

Kulingana na stakabadhi hizo Nyachae alinunua ekari 17.815 za ardhi mwaka 2006 kwa shilingi 343,000 licha ya kwamba shamba hilo halikuwa linauzwa.

Gideon Toroitich alikuwa meneja mkurugenzi wa ADC na alikuwa na uhusiano na familia ya Moi.

Aliyekuwa mwandani wa Rais Mustaafu Daniel Moi na mwanasiasa shupavu Ezekiel Barng’etuny pia alipata ekari 14 za ardhi hiyo mwaka 1995 kwa shilingi 288,000.

Miongoni mwa majina ya watu tajika walionufaika kwa kugawiwa ardhi hiyo kinyume na sheria ni aliyekuwa waziri Noah Katana Ngala, waziri wa zamanai marehemu Kipkalya Kones, aliyekuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Egerton James Tuitoek, Aliyekuwa waziri msaidizi Abubakary Badawy na mbunge wa zamani Jonathan Katana Nzai.

NA LUKE AWICH