Wandani wa Ruto wadai kuwepo njama ya kutumia 'Huduma Namba' kwa sababu za kisiasa

Takriban wabunge 40 wa chama tawala cha Jubilee wametoa tahadhari kuhusu kuwepo kwa njama ya kuvuruga data kupitia Huduma Namba kwa sababu za kisiasa.

Wabunge waliokuwa wameandamana na naibu rais katika ziara eneo la Kajiado siku ya Alhamisi, walidai kwamba watalaam walikuwa wameajiriwa kusimamia awamu ya pili ya usajili wa Huduma Namba.

Walihoji usiri unaogubika usajili huu, zabuni ambayo wanasema ingetangazwa hadharani.

“Mbona idara ya NIS inahusishwa katika mapendekezo ya usajili badala ya wizara husika ?” aliuliza seneta wa Nakuru Susan Kihika.

Alisema kwamba wito wa kufanyika kwa awamu ya pili ya kuwasajili wakenya kwa Huduma Namba ni utapeli, kama tu sakata ya coronavirus ambapo mabilioni ya pesa za walipa ushuru zilifujwa.

“Wakenya wamechoka na serikali hii fisadi. Hii ndio sababu tunaunga mkono kuvunjwa kwa bunge kama alivyoshauri Jaji Mkuu,” Kihika aliongeza.

Seneta huyo alisema wakati umeawadia kwa serikali kujiuzulu.

Mbunge wa Kimilili Didmus Baraza alisema kwamba nchi haiwezi kuendelea kupoteza pesa wakati huu ambapo wakenya wengi wanapitia wakati mgumu kiuchumi.

“Pesa nyingi zilitumika katika awamu ya kwanza ya usajili wa Huduma Namba. Hatuwezi kuendelea kupoteza pesa kwa miradi ambayo haina manufaa kwa umma,” Barasa alisema.

Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung'wa alisema kwamba kamwe hawatakubali sakata nyingine kufanyika kwa kisingizio cha kusajili watu.

Usemi huu uliungwa mkono na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, seneta maalum Millicent Omanga, mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na mwenzake wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali.

Wabunge hao walisema kwamba wakenya wanataka kujua nini kilifanyika kwa awamu ya kwanza ya usajili wa Huduma Namba.