Wandani wa Ruto watofautiana baada ya William Ruto kutoa kadi yake ya kisiasa

Sasa ni wazi kuwa huenda Naibu Rais William Ruto akajiondoa kutoka chama cha Jubilee na kuingia chama chake. Hilo lilidhihirika Alhamisi, Juni 18, wakati DP Ruto alikutana na wabunge 16 katika afisi za Jubilee Asili Centre.

Inaaminika DP William Ruto ameunda chama hicho atakachowania urais nacho ifikapo 2022 baada ya masaibu kumzidi ndani ya Jubilee.

DP ndiye naibu wa chama cha Jubilee huku Rais Uhuru Kenyatta akiwa kiongozi wa chama. Hata hivyo, DP amekuwa akipokea kichapo kikali kisiasa kutoka kwa maafisa wengine kama vile katibu Raphael Tuju na naibu mwenyekiti David Murathe.

"Nimekuwa na chakula cha mchana na wabunge wa Jubilee ambao hivi karibuni walitolewa kwenye nyadhifa zao na kupewa wajibu mwingine. Niliwashukuru kwa kazi yao kwa chama na taifa," alisema DP kuhusu mkutano wake na wabunge hao katika makao ya Jubilee Asili.

Huku kauli mbiu ya chama cha Jubilee ikiwa ni 'Tuko Pamoja', DP alimalizia ujumbe wake 'Sote Pamoja' katika kile kiliashiria usemi wa chama hicho kipya.

Hatua ya DP ilijiri siku moja tu baada ya Murathe na Tuju kuongoza Jubilee kutia sahihi mkataba wa ushirikiano na chama cha Wiper na CCM.

Hatua ya DP inatarajiwa kuzua hisia kali za kisiasa ndani ya Jubilee wakati ambapo Rais Kenyatta anaonekana kutangaza vita dhidi ya wandani wa Ruto.

Tayari Jubilee Asili ina ukurasa wa Facebook ambapo picha ya DP imewekwa na kutangazwa kama chama cha kisiasa.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, hata hivyo, alisema Jubilee Asili si chama kingine mbali ni nyumba ya wanaoamini kuhusu ajenda ya awali ya Jubilee.

"Tulikuwa na mkutano na DP katika jumba la Jubilee Asili Centre. Ni makao ya wanachama wote si chama mbadala kwa Jubilee

Ni makao ya wanachama wanaoamini kuhusu ajenda ya awali ya Jubilee." Murkomen alisema.

Hata hivyo, Mbunge wa Soy Caleb Kositany ambaye pia ni naibu katibu wa Jubilee alisema kuna mipango ya kusajili Jubilee Asili kama chama cha kisiasa.

"Sisi kwa Jubilee hakuna demokrasia, hakuna tena kujadiliana, imekuwa ni kama klabu ya watu wachache ambapo wanachama wanaamriwa kile watafanya. Kama hawatapinga kusajiliwa, basi tutakuwa na chama cha Jubilee Asili." Alisema Kositany.