Wataalam wa afya wamshauri Uhuru kutofunga nchi kwa sababu ya corona

Uhuru
Uhuru
Wataalam wa afya wamemshauri rais Uhuru Kenyatta kupuuza wito wa kutoa amri ya kutotoka nje kabisa ili kudhibiti usambaaji wa virusi vya corona.

Uhuru amekuwa akipokea shinikizo kutoa agizo la kusitisha kabisa shughuli za kawaida nchini. Hii inafuatia kuongezeka marudufu kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Habari zaidi;

Rais Kenyatta ameitisha mkutano na magavana siku ya Jumatatu kujadili athari za kulegezwa kwa masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi hivi.

Kuna dalili kuwa huenda masharti mapya makali yakatangazwa hasa baada ya wizara ya elimu kuamuru maafisa wake kutosafiri nje ya Nairobi.

Rais Kenyatta vile vile aliagiza mawaziri wake wote kutoongoza ujumbe wowote katika ukaguzi wa miradi ya serikali.

Duru zilidokezea Radio Jambo kwamba serikali imekuwa ikitathmini uwezekano wa kusitisha shughuli kabisa, lakini wataalam wa afya wamepinga hatua hiyo.

Habari zaidi;

Mark Nyanyingi, mtaalam wa usambaaji wa maradhi,  Dkt Mohamud Sheik aka Omar, mtaalam wa magonjwa ya kuambukizana ambaye pia ni mbunge wa Wajir South na Afisa mkuu mtendaji wa shirika la Amref Health Africa Dkt Githinji Gitahi walipinga vikali hatua ya kufunga shughuli kabisa.

Walisema kwamba hatua hii imepitwa na wakati kwa sababu maambukizi sasa yamekita mizizi katika jamii.

“Maambukizi ya Covid-19 hufanyika ndani ya nyumba na sio kwa barabara. Yanafanyika mahali mtu anakaa kwa muda mrefu na mara nyingi,” alisema Nyanyingi

Alitoa mfano wa Marekani ambapo utafiti ulionyesha kwamba asilimia 70 ya maambukizi yalifanyika ndani ya nyumba.

Nyanyingi aliongeza kwa kutoa wito kuimarishwa kwa shughuli za kutafuta watu waliokaribiana na wahasiriwa akisema kwamba pamekuwepo na ulegevu katika kuendeshwa kwa zoezi hilo.

“Pia tunahitaji kuimarisha mikakati ya kuwakinga watu walio na mardhi mengine au tuyape mahitaji yao kipau mbele.”

“Nilikuwa naungo mkono kufungwa kabisa kwa shughuli zote lakini ugonjwa huu umebadili mkondo na hatujaweka mikakati ambayo ingetusaidia kudhibiti ugonjwa huu,” Nyanyingi alisema.

Habari zaidi;

Dkt Omar (Mbunge wa Wajir South) alisema kufungwa kwa shughuli za kawaida kwa sasa hakuwezi kusaidia sana na kuongeza kuwa homa ya Influenza ya mwaka 2019 iliathiri watu wengi sana kuliko corona.

“Katika sayansi tunaamini kwa kinga thabiti ya mwili na kinga ya kiasili ndio watu sasa wanahitaji. Katika lugha ya kawaida ‘nikinge, ili nikukinge’,” mbunge huyo alisema.