Watu 147 wamepatikana na virusi vya corona Kenya - Mutahi Kagwe asema

Kati ya watu 2831 waliofanyiwa vipimo vya kubaini virusi vya corona nchini, watu 147 wamepatikana na virusi vya corona  na kufikisha idadi ya watu walioathirika Kenya kuwa 1618.

Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema miongoni mwa waathiriwa hao wapya ni kati ya mwaka 1 hadi 77.

Ametangaza kuwa hii leo serikali imeruhusu wagonjwa wengine 13 na kufikisha idadi ya watu waliopona kuwa 421.

Aidha, taifa limewapoteza wagonjwa wengine watatu waliopoteza maisha kutokana na virusi hivyo na kufikisha idadi ya watu waliokufa kuwa 58.

Visa hivyo vipya 147 katika kaunti ya Nairobi vimetokea maeneo yafuatayo, Kibra35 - Langata15 - Makadara 9 - Westlands 8 - Kamkunji2 - Mathare 1.

Nairobi imesajili visa 90 kati ya 147 huku kaunti ya Mombasa ikisajili visa 41.

Kati ya kaunti 47 za humu nchini, kufikia sasa majimbo 32 yamesajili visa vya corona.

Mutahi pia ametangaza kuwa serikali imetanga shilingi milioni 216 kama njia ya kufanikisha shughuli katika hospitali ya Kiambu ambapo baadhi ya wagonjwa wametengwa.

Mutahi pia amesifia pakubwa hatua ya uongozi wa gavana James Nyoro kuwaajiri wahudumu wa afya 200 akisema ni sharti wakuu wengine wa kaunti kufuata mkondo huo.

Amewataka wananchi kuacha kuendeleza unyanyapaa miongoni mwa wagonjwa ambao wanapona dhidi ya virusi hivyo.

Vile vile kati ya visa 147 vilivyoripotiwa hii leo, wanaume walikuwa 87 huku wanawake wakiwa 60.

Kaunti zingine ziklizosajili visa vya maambukizi ni  Kiambu 3,  Nyeri na  Uasin Gishu zote zikiwa na wagonjwa wawili.

Mkurugenzi wa afya Dr Patrick Amoth amesema kwa sasa taifa la Kenya liko na wagonjwa 692 [active cases] huku watatu kati yao wakiwa katika hali mahututi.