Watu 5 wahukumiwa kifo kwa mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi

khashoggi
khashoggi

Mahakama moja nchini Saudi Arabia imewahukumu watu watano kifo na kuwafunga wengine watatu baada ya kuwapata na hatia ya mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi mwaka jana.

Khashoggi, alikuwa mkosoaji kinara wa serikali ya kifalme ya Saudia aliuawa ndani ya ofisi ndogo ya ubalozi wa nchi hiyo katika Jiji la Istanbul, Uturuki mwaka 2018.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Saudia amesema mauaji hayo yalikuwa ni sehemu ya "operesheni haramu" na kuwashtaki watu 11 ambao hata hivyo majina yao hayakuwekwa wazi.

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa (UN) alifikia hitimisho kuwa yalikuwa "mauaji ya serikali yasiyofuata utaratibu."

Mtaalamu huyo Agnes Callamard pia alipendekeza kwenye ripoti yake kuwa Mwanamfalme Mohammed bin Salman achunguzwe kutokana na mauaji hayo.

Bin Salman hata hivyo amekanusha kuhusika kwa namna yeyote ile, lakini mwezi Oktob mwaka huu akasema kuwa "anawajibika moja kwa moja akiwa kama kiongozi wa Saudia, na hususani kwa kuwa mauaji hayo yametekelezwa na maafisa wa serikali ya Saudia."

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema kuwa kesi hiyo haikukidhi viwango vya kimataifa na mamlaka za nchi hiyo "zilizuia njia zote stahili za uwajibikaji".

Jamal Khashoggi alikufa vipi?

Mwandishi huyo aliyekuwa na miaka 59 alipofikwa na umauti alikuwa akiishi Marekani na kuandika maoni kwenye gazeti maarufu la Washington Post.

Mara ya mwisho kounekana akiwa hai ilikuwa Oktoba 2, 2018 akiingia kwenye ofisi ndogo za ubalozi wa Saudia ili kuchukua karatasi zake za talaka.

Alikuwa mbioni kumuoa mpezi wake wa Kituruki Hatice Cengiz.

Baada ya kusikiliza kanda za sauti zilizonaswa na maafisa wa usalama wa taifa wa Uturuki, Bi Callamard alifikia hitimisho kuwa Khashoggi "aliuawa kinyama" siku hiyo.

Naibu mwendesha mashtaka wa Saudia Shalaan Shalaan aliwaambia wanahabari Novemba 2018 kuwa mauaji yaliamriwa na mkuu wa "timu ya mapatano" iliyotumwa Istanbul na mkuu msaidizi wa idara ya usalama wa taifa ya Saudia kwa kazi ya kumrejesha Khashoggi nyumbani "kwa jia ya ushawisi" na edapo hilo lingeshindikana, "basi kwa nguvu.

Wachunguzi pia walifikia hitimisho kuwa Khashoggi alifungwa kwa lazima ma kisha kukabwa koo na kamba kabla ya kudungwa sindano lukuki za dawa ambazo zilipekea kifo chake. kwa mujibu wa bw Shalaan.

Baada ya hapo mwili wake ulikatwa katwa vipande na kukabidhiwa kwa mshirika wa kituruki nje ya ubalozi. Mabaki hayo hayajapatikana tena.

Bw Shalaan hata hivyo anasisitiza kuwa Mwanamfalme Mohammed "hakuwa na habari yeyote juu ya tukio hilo".

-BBC