Watu 54 Kenya wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kupata nafuu kutokana na corona

EZlw9srXkAAGeHm.jfif
EZlw9srXkAAGeHm.jfif
Katibu msimamizi katika wizara ya afya Dr Rashid Aman amesema kwa mara ya kwanza nchini, Kenya imewaruhusu watu 54 waliokuwa wamelazwa hospitalini kutokana na virusi hivyo hatari kurudi nyumbani baada ya kupata nafuu.

Idadi hiyo mpya sasa ya watu walioruhusiwa kuondoka hospitalini inafikisha watu 553.

Aman amesema asilimia kubwa ya wakenya sasa wamerejelea hali yao ya kawaida hatua ambayo amesema inaweza kuliweka taifa hatarini.

Amesifia pakubwa hatua ya idadi kubwa ya wakenya ambao wanaendelea kuzingatia masharti ya serikali.

Amesema idadi kubwa ya madereva inayoendelea kushuhudiwa katika mipaka ya Kenya ni kutokana na baadhi yao kukosa vyeti vya kuonyesha hali yao ya afya kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini.

Wakati uo huo, Aman amesema watu 123 wamepatikana na virusi vya corona baada yaa kufanyiwa vipimo na kufikisha watu 2216.

Jimbo la Nairobi limesajili visa 44  na Mombasa visa 34.

Aman pia amesema taifa limepoteza wagonjwa wengine watatu na kufikisha idadi ya watu waliokufa nchini kuwa 74.

Visa 20 vilivyoripotiwa katika jimbo la Busia vimetokana na madereva wa malori ya masafa marefu waliopimwa mipakani.

Kaunti ya Kajiado vile vile imeripoti visa vingine vitatu huku wagonjwa hao wakiwa madereva kutoka kwa mpaka wa Namanga.

Mvulana wa miaka 12 ni miongoni mwa watu watatu waliofariki hii leo kutokana na virusi hivyo.

Kuhusiana na idadi ya watu waliozuiliwa katika maeneo mbalimbali ya karantini nchini, Aman amesema serikali inaweka mikakati ya kuhakikisha kuwa inatoa matokea yao kwa muda.

Serikali imeanzisha mchakato wa kuwapima mahabusu wote katika magereza yaliyoko kaunti ya Nairobi  baada ya kuripotiwa kwa visa vya maambukizi .

Kufikia sasa, serikali imewapima wakenya 85,058 kutokana na virusi vya corona.