Watu sita wauawa na umati katika kaunti ya Busia

Watu sita Ijumaa walipigwa hadi kufa na umati uliokuwa na ghadhabu katika kaunti ya Busia.

Sita hao hawakutambuliwa na wenyeji mara moja na wanasemekana  kukodiwa na mwanamke mmoja mfanyabiashara ili kuchukua mwili wa mwanaume mfanyabiashara  aliyekuwa ametekwa nyara na baadaye mwili wake kupatikana katika kijiji cha Marachi.

"Wakaazi waliwashuku walipowaona sita hao wakiwa wamevalia suti nyeusi. Mmoja wao aliyekuwa na begi aliamrishwa kutwaa likaguliwe na ndani yake likapatikana visu vitatu," kamanda wa polisi kutoka Magharibi Edward Mwamburi alisema.

"Wanakijiji waliwashuku kwamba huenda watu hao walihusika na kifo cha mfanyabiashara huyo na kuwashambulia hadi wakafa."

Mfanyabiashra John Aduor alitekwa nyara nyumbani kwake Masebula na watu watatu ambapo mmoja wao alikuwa amejihami na bunduki na baadaye Aduor kupatikana ameaga dunia katika Kagonya, kaunti ndogo ya Ugenya.

Kisa hicho kilitokea katika shule ya msingi ya Wamasela ambapo mwili wa mfanyabiashara huyo ulikuwa unatazamwa na umma Ijumaa jioni kabla ya mazishi.

Hafla ya mazishi ilikuwa imepangwa kufanyika Jumamosi katika wadi ya Marachi Magharibi.

Sita hao wanaaminika kuwa vijana wa kukodiwa na wanasiasa katika Ugenya.

"Tumeanza uchunguzi wetu na yeyote atakayepatikana kutekeleza mauaji hayo atakumbana na mkono wa sheria," Mwamburi alisema.

Aidha aliwaonya umma dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao.