Watu watatu wauawa huku watatu wakijeruhiwa Alshabab waliposhambulia basi Lamu

unnamed-compressed
unnamed-compressed
Watu watatu wamethibitishwa kuuawa kufuatia shambulizi la basi katika kaunti ya Lamu Alhamisi alfajiri.

Kamishina wa kaunti ya Lamu Irungu Macharia kwenye mawasiliano ya simu na Radio Jambo alisema kuwa wapiganaji wanaoshukiwa kuwa wa Alshabab waliwauwa watu watatu kwa kuwafyatulia risasi na kuwajeruhi wengine watatu katika eneo la Nyongoro, barabara ya Lamu-Garsen.

Macharia alisema kuwa vikosi vya kulinda usalama wametumwa katika eneo hilo kuwakabili majangili hao.

Aidha, alisema kuwa huenda idadi ya maafa ikaongezeka kutokana na majeruhi mabaya kwa wahasiriwa.

"Nimethibitisha kuwa watu watatu wamefariki dunia baada ya wapiganaji kufyatulia risasi basi walimokuwa wakisafiria. Wengine  watatu wameponea kifo ijapokuwa kwa majeraha mabaya zaidi. Tutawapa taarifa zaidi pindi uchunguzi utakapokamilika.," Macharia alisema.

Taarifa zinasema kuwa kikundi cha wapiganaji  walijitokeza kwenye msitu na kuamuru dereva wa basi  hilo  kusimamisha, lakini dereva aliposhuku kuwa walikuwa majangili, aligaidi amri na kuendesha gari hilo kwa kasi, hapo ndipo walipomiminia basi hilo risasi kadhaa.

Basi hilo linalomilikiwa na kampuni ya Mombasa Raha lilitoka Lamu 7.30 asubuhi likielekea Mombasa kabla ya kuvamiwa.

Akizungumza na Radio Jambo, mfanyakazi mmoja wa huduma za Mombasa Raha alisema kuwa basi hilo lilikuwa na abiria 44 pamoja na dereva kabla ya kushambuliwa.

Eneo la Nyongoro ni kati ya maeneo yanayosemekana kuwa hatari sana kutokana na hali mbaya ya barabara na pia upungufu wa hali huduma za mawasiliano ya simu.

Kwa sasa huduma katika eneo hilo zimesimamishwa huku maafisa wa usalama wakianzisha uchunguzi.