Wawili wauliwa, 6 watiwa mbaroni kwa mizozo ya ardhi

police
police
Watu wawili waliuliwa Jumapili usiku katika mzozo ulioanza upya baina ya vikundi viwili vinavyozozania ardhi huko Lolgorian, Transmara Magharibi.

Mauaji hayo yalizua maandamano ya wakaazi huko Kilgoris Jumatatu huku wakilalamikia kuzorota kwa usalama. Polisi wanahoji watu 6 waliotiwa mbaroni kuhusiana na machafuko hayo yaliyohusisha koo mbili.

Koo hizo zinaaminika kupigania juu ya mpaka wa Nkaararo-Enosaen.

Katika maandamano ya jana, takribani watu 30 walitiwa mbaroni na kuachiliwa baadaye.

Wenyeji hao wanasema watu zaidi wanaweza kuuliwa iwapo serikali itashindwa kuchukua hatua za haraka na kumaliza mgogoro huo.

Mzozo huo ambao umedumu kwa zaidi ya miongo miwili na umewasababishia wanakijii maafa mengi, majeraha mabaya na huku wengine wakihama na kutoroka makwao.

Vijana wengine wanadaiwa kuuliwa kwa kupigwa risasi na polisi wanaotumwa kumaliza mvutano.

Mnamo Jumatatu, zaidi ya waandamanaji mia tatu, haswa wanawake, walijitokeza kwenda Kilgoris kuomba serikali kumaliza vurugu hizo.

Kamishna wa kaunti ya Transmara magharibi Hassan Noor alisema vikosi vya usalama vikiwemo GSU, kitengo cha askari wa kupambana na wizi wa mifugo na polisi wa kawaida wamepelekwa katika eneo hilo.

"Tunafanya kila kitu kuhakikisha kuwa suala hili la mpaka linashughulikiwa haraka ili watu warejee katika makaazi yao." Noor alisema.

"Waliokamatwa watapelekwa mahakamni Jumanne ikiwa tutapata ushahidi wa kutosha," Noor alisema.

Alisema kikosi cha masoroveya kutoka Nairobi wameitwa ili kutatua na kumaliza mizozo ya ardhi.

"Kwa kweli tunangojea ripoti kutoka kwao wiki hii. Tunatumaini kuwa ikiwa itatekelezwa, ripoti hiyo itamaliza mzozano kati ya pande hizo mbili."

Aidha alsiema kuwa mili ya waliouliwa katika mashambulizi hayo ilipelekwa katika mochari ya hospitali ya kaunti ndogo ya Kilgoris.