Waziri mkuu wa Uganda ajiweka karantini baada ya kutangamana na watu waliopatikana na corona

25037270_161828917922175_996136141532954624_n
25037270_161828917922175_996136141532954624_n
Waziri Mkuu wa Uganda Ruhakana Rugunda amejiweka karantini baada ya watu aliotangamana nao kupatikana na virusi vya COVID-19.

Rugunda alisema hakupatikana na virusi hivyo baada ya kupimwa ila ameonelea ni vyema kufuata masharti yaliowekwa ya kudhibiti maambuki ya virusi hivyo.

" Marafiki zanguni, nimeamua kujitenga kwa siku 14 baada ya watu niliotangamana nao kukutwa na virusi vya COVID-19, mimi mwenyewe sijapatikana na virusi hivyo lakini nafuata masharti yaliowekwa na wizara ya afya ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huu," Alisema Rugunda.

Wizara ya afya nchini humo  Alhamisi, Juni 4 ilitangaza  kuwa sampuli 2,267 zilifanyiwa vipimo na visa vyote ni vya raia wa Uganda.

Kufikia sasa nchi hiyo imethibitisha visa 35 vipya vya maambukizi ya virusi vya COVID-19 chini ya saa 24 zilizopita na kufanya idadi ya walioambukizwa kufikia 557.

Aidha, madereva 31 wa malori, 18 wakiwa Wakenya, 7 Watanzania, 4 Wakongo na 2 Waburundi waliopatwa na virusi hivyo walirejeshwa makwao.