Waziri wa elimu afutwa kazi Madagascar kwa kuagiza lollipop za dola milioni 2

_112736397_gettyimages-1224893134_crop (1)
_112736397_gettyimages-1224893134_crop (1)

Waziri wa elimu nchini Madagascar amefukuzwa kazi kwa sababu ya mipango yake ya kuagiza peremende au pipi zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 2 sawa na (£1.6m) kwa watoto wa shule.

Rijasoa Andriamanana amesema wanafunzi watapewa pipi tatu kila mmoja watakazokula baada ya kunywa dawa ya mitishamba inayodaiwa kutibu virusi vya corona nchini humo ambayo bado haijathibitishwa.

Mpango huo ulitupiliwa mbali baada ya kupingwa na rais wa Madagascar.

Rais Andry Rajoelina anapigia debe dawa ya mitishamba walioibaini kama yenye uwezo wa kutibu virusi vya corona.

Nchi kadhaa za Afrika zinaendelea kuagiza dawa hiyo ya mitishamba inayoaminiwa kusaidia katika kukabiliana na virusi vya corona lakini Shirika la Afya Dunia (WHO) limeonya kuwa dawa hiyo bado haijathibitishwa kuwa na uwezo huo.

Taasisi ya Taifa ya Matibabu nchini Madagascar pia nayo imetilia shaka uwezo wa dawa hiyo inayotokana na mmea wa pakanga yaani (Artemisia) ikisema kwamba inaweza kusababisha matatizo ya afya kwa watu.

Rais Rajoelina amepuuzia ukosoaji juu ya dawa hiyo ya mitishamba, akisema ni wazi kuwa nchi za magharibi inadharau uwezo wa Afrika.

"Kama ingekuwa ni nchi ya Ulaya ambayo imegundua dawa hii, Je kungekuwa na mashaka kiasi hiki, Sidhani," aliambia chombo cha habari cha Ufaransa cha France 24.

Karibia watu 1,000 wamethibitishwa kupata virusi vya corona nchini humo, pamoja na vifo saba ambavyo vinahusishwa na virusi hivyo.

-BBC