Wenye majumba jijini Nairobi wapewa siku 14 kuyapaka rangi

Kaunti ya Nairobi itawachukulia hatua kali za kisheria wenye majumba katikati mwa jiji ambao hawatakuwa wameyapaka rangi  upya katika muda wa siku 14 kuanzia leo  (Jumatano).

Serikali ya kaunti tayari imewajulisha wenye majumba kuzingatia sheria ya afya ya umma kipengele cha 242 na kanuni za serikali ya kaunti. Kulingana na sheria hizo majumba yote katikati mwa jiji yanafaa kupakwa rangi upya kila baada ya miaka miwili.

Habazi zaidi :

Kaimu katibu wa kaunti na mkuu wa utumishi wa umma katika kaunti ya Nairobi Leboo Morintat, katika ilani kwa wenye majumba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wamiliki wa majengo ambao hawatakuwa wametekeleza agizo hilo.

"Ili kuimarisha urembo wa jiji, wenye majumba katikati mwa jiji la Nairobi wanatakiwa kuyasafisha/kuyapaka rangi au kuyarembesha kuambatana na sheria," ilani hiyo ilieleza. Wenye majengo pia wamepewa idhini kurembesha sehemu zilizoko mbele ya majumba yao ili yawe maridadi na ya kuvutia. Hili ni eneo kati ya nyumba na barabara.

Habari zaidi:

Kaimu katibu wa kaunti aliapa kuhakikisha upakaji rangi majumba unafanywa kwa kiwango kinachohitajika.

Leboo alisema kwamba jiji la Nairobi limetambulika kimataifa kama mji thabiti, wenye ubunifu na wenye ustahilivu na hivyo unafaa kulindwa ili kusalia katika hadhi hiyo.

Mwenyekiti wa kamati ya bunge la kaunti kuhusu nyumba Antony Karanja alisema kwamba sheria za kaunti zinahitaji kila jengo katikati mwa jiji kupakwa rangi kila baada ya miaka miwili.

Mapema mwaka huu, Gavana wa Nairobi Mike Sonko alitowa wito kwa wamiliki wa majumba katikati mwa jiji la Nairobi kuyarembesha ili kuhakikisha kwamba jiji linasalia na hadhi yake.

"Twafahamu jiji la Nairobi ni chagua la wawekezaji, wafanyikazi na wale wanaotaka kuishi lakini tunafaa kuweka juhudi kuimarisha hadhi yake katika kanda hii na kimataifa," alisema wakati akikagua zoezi la jiji la Nairobi.

Mji wa Nairobi mwezi uliyopita ulituzwa mji bora barani Afrika katika biashara na utalii katika halfa ya World Travel Awards mwaka 2019 nchini Mauritius.