Yaliyomo: Njama ya Ruto kutema chama cha Jubilee, mipango ya 2022

ruto-sued-660x330
ruto-sued-660x330
Taarifa kuwa chama tawala cha Jubilee kimegawanyika kuwili sio habari mpya kwa sasa.

Ndoa hii ya Jubilee imekumbwa na songombingotele.

Kuvunjika kwa ndoa hii ni ishara ya usaliti wa vyama vya kisiasa nchini.

Muungano wa NASA ulisambaratika kitambo.

Dalili zote zipo kuonyesha Ruto na Uhuru hawasafirii chombo kimoja.

Hii inadhihirika wazi na jinsi mikutano yao katika eneo mlima Kenya zinagongana.

Mkutano wa leo wa Uhuru Kenyatta na viongozi wa eneo la mlima Kenya umeibua maswala mapya ambayo hayakukusudiwa.

Nyufa zimeonekana waziwazi kuwa huenda ofisi ya Ruto na Uhuru hazina mipangilio mwafaka na zinakosa kushauriana kuhusu mikutano.

Ruto alikuwa na hafla yake Nyeri na kuisitisha baada ya taarifa kuwa Uhuru atakuwa na mkutano Sagana.

Ziara hii imewekwa kando ili kumpisha Rais Kenyatta kufanya kikao na wabunge wa mlima Kenya.

Wachanganuzi wa siasa wanahoji kuwa huenda uhusiano wa karibu uliokuwepo wa viongozi hawa wawili ulikatika ghafla baada ya wandani wa Uhuru kugundua ngome yake inavamiwa na wabunge kugeuza ufuasi wao kwa Ruto.

Kinachoshangaza wengi ni kuwa kuna wafuasi wa TangaTanga ambao wameibua taarifa kuwa kuna mipango ya Ruto kuitema Jubilee.

Kwa upande mwingine, Ruto anaonekana sana kuweka mambo sawa na kulazimisha ndoa ya Jubilee kuendelea.

Ruto ana nafasi na haki ya kujiuzulu iwapo atahisi kuwa ananyanyaswa katika ndoa hii.

Wabunge watatu wamenukuliwa kusema kuwa Ruto anapania kuitema Jubilee kwa misingi kuwa haoni mustakabali mwema wa ndoto yake ya kisiasa na mrengo huu.

Ikumbukwe kuwa iwapo Ruto atafanya hivi, atakuwa makamu wa rais wa kwanza kufanya hivyo katika historia ya Kenya.

Wabunge hawa walidokeza kuwa hali ngumu ya maisha iliyopo kwa sasa pamoja na hali duni ya uchumi ni kati ya vitu vinavyomfanya naibu wa rais kuiogopea zaidi 2022.

Kuna madai kuwa Ruto analenga sana kutumia Chama Cha Mashinani (CCM) chake aliyekuwa gavana wa Bomet Isaac Ruto ifikapo 2022.