Zaidi ya vyuo 50 vya kiufundi vyapata wasimamizi wapya

Jwan
Jwan
Zaidi ya vyuo vikuu 50 vya kiufundi vitapata wakuu wapya katika mabadiliko yaliyotangazwa na wizara ya elimu idara ya vyuo vya anuai.

Vyuo vya Rift Valley Technical Training Institute, Siaya Institute of Technology, Meru National Polytechnic, Nyandarua TTI, P.C Kinyanjui, KTTC, Taasi ya Kiambu ni miongoni mwa vyuo ambavyo zimeguswa na mabadiliko hayo mapya.

Katika mabadiliko hayo, Edwin Tarno aliyekuwa mkuu wa chuo cha Rift Valley Technical Training Institute sasa amehamishiwa katika chuo cha KTTC.

John Odhiambo amehamishwa kutoka Siaya TTI hadi Kabete National Polytechnic huku Stephen Ntarangwi aliyekuwa kaimu naibu wa mkuu wa Meru National Polytechnic amepandishwa daraja na sasa atakuwa mkuu wa chuo hicho.

Katibu wa kudumu wa vyuo vya anuai Julius Jwan alisema siku ya Jumanne kwamba mabadiliko hayo yataleta sura mpya katika vyuo hivyo na kujaza pengo liliko kati ya mafunzo na ukuzaji wa ujuzi wa kiufundi na teknolojia.

Jwan alisema sekta ya kiufundi imesalia kupuuzwa  na kutotumiwa kikamilifu. Kutokana na hali hii wanafunzi wengi wamekuwa wakitoroka vyuo vya kiufundi vya serikali kutokana na mtaala duni usiowapa matumaini ya kujiendeleza maishani.