Spika wa bunge Justin Muturi katika arifa kwa wabunge amesema matokeo ya waliopimwa kutoka bunge na seneti pamoja na wafanyikazi wa mabunge yote yameonyesha kwamba hakuna aliyepatikana na virusi hivyo.
“ Ningependa kusisitiza kwamba matokeo haya hayafai kutufanya tulegeze kamba kuhusu jitihada za kudumisha usafi na kuwa na tahadhari pamoja na kuvalia barakoa na kuepuka maeneo yaliyo na misongamano.’ Muturi alishauri.
Vipimo vya hiari vya wabunge na wafanyikazi wa bunge vilifanywa kati ya Aprili tarehe 2 na tarehe 4 katika majengo ya bunge.
Bunge liliwataka wajumbe na wafanyikazi kufanyiwa vipimo kwa hiari kama jitihada za mapema za kukabiliana na ugonjwa huo baada ya ripoti za magazeti kudai kwamba wabunge 17 wamepatikana na virusi hivyo.
Muturi amesema tume ya wafanyikazi wa bunge inandaa vipimo vinginge kwa wabunge na wafanyikazi wa bunge na wanafaa kuendelea kufuata ushauri na mwongozo unaotolewa na shirika la afya duniani WHO na wizara ya Afya nchini
“ Shughuli hiyo itakuwa ya hiari na inawalenga wabunge wote na wafanyikazi. Wengine watakaopimwa ni wafanyikazi waliopewa kandarasi ya kufanya kazi ya usafi bungeni. ‘ Muturi aliongeza