Jose Chameleone asherehekea kufikisha miaka 45 kwa kumbukumbu ya marememu kakake

Humphrey Mayanja aliaga dunia Machi 30, mwezi mmoja kabla ya siku ya kuzaliwa ya kakake mdogo na Chameleone alijisherehekea kwa video za zamani kakake akimtumia heri njema za kuzaliwa.

Muhtasari

• Chameleone alifichua kwamba amefikisha umri wa miaka 45 na kumtaka kakake kupumzika pahali pema palipo wema.

Jose Chameleone
Jose Chameleone
Image: Instagram

Joseph Mayanja, maarufu kama Jose Chameleone amesherehekea kufikisha umri wa miaka 45 kwa kumbukumbu nzuri ya marehemu kakake Humphrey Mayanja ambaye amefariki wiki chache zilizopita.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Chameleone alichapisha video ya Humphrey Mayanja akimsifia na kusema kwamba ndiye alikuwa kakake ambaye walifanya mambo mengi pamoja.

Chameleone alifichua kwamba amefikisha umri wa miaka 45 na kumtaka kakake kupumzika pahali pema palipo wema.

“Asante Humphrey kwa maisha mazuri na yote uliyochangia kwangu kama kaka yako mdogo. Tulipigana, tukabishana, tukakubaliana. Zaidi ya yote tulipendana - Pumzika vizuri papa. Nina umri wa miaka 45 leo. Mpaka tukutane tena baba,” Chameleone aliandika.

Katika video hiyo ya kakake Humphrey, alikuwa akizungumza kwa kumsifia mdogo wake wakati wa siku yake ya kuzaliwa miaka ya nyuma huku akimtakia siku njema ya kuzaliwa.

“Yoh yoh yoh, Joseph Mayanja Chameleone, ni siku yako ya kuzaliwa kaka, jivinjari. Nakupenda na nakumiss sana. Heri njema ya kuzaliwa kaka, nakupenda na kuwa salama,” Humphrey alizungumza katika video hiyo.

Humphrey Mayanja aliaga dunia Machi 30 alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali moja nchini Uganda. Alikuwa na maumivu makali ya tumbo na ilimbidi afanyiwe upasuaji.

Babake Gerald Mayanja alifichua kuwa alikuwa akitibiwa saratani ya koloni ya hatua ya 4 mwanzoni mwa Machi.

Chameleon alikuwa amechapisha picha ya kakake kwenye mitandao yake ya kijamii akiisindikiza na emoji za kulia huku akitangaza kufariki kwake ghafla. Mashabiki wake walimiminika kwenye sehemu ya maoni huku wakimfariji.