Mwanahabari wa kimataifa wa Kenya Larry Madowo amethibitisha kuwa bado anafanya kazi katika kampuni ya habari ya Cable News Network. (CNN).
Hapo awali, mtangazaji huyo wa zamani wa NTV alikuwa amedai kwamba amerejea katika kampuni ya habari aliyofanyia kazi katika siku za nyuma BBC Washington, jambo ambalo sasa amefichua kuwa ni mzaha uliokusudiwa kwa Siku ya Wajinga duniani mnamo Aprili 1.
Madowo alijivunia kukaa kwake kwa miaka mitatu katika CNN na kusema kwamba tayari amerejea BBC ambako alifanya kazi hadi 2020.
"Habari kiasi za kibinafsi: baada ya miaka 3 ya kusiskimua na CNN, nina furaha kushiriki kwamba nimerejea BBC jijini Washington.
Asante kwa safari nzuri ������,” Larry Madowo alisema Jumatatu asubuhi kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.
Saa chache baadaye, hata hivyo, mwanahabari huyo mzoefu hata hivyo alithibitisha kwamba bado yuko CNN na kufafanua kwamba alikuwa akiwatania tu mashabiki wake.
Alifichua kuwa picha yake akiwa katika studio za BBC aliyoshiriki katika chapisho lake la kwanza ilipigwa miaka mitatu iliyopita alipokuwa bado anafanya kazi katika shirika hilo la habari.
"Huu ulikuwa mzaha wa Siku ya Wajinga wa Aprili. Bado niko na CNN. Lakini kazi yangu ya mwisho ilikuwa na BBC huko Washington, na hii ni picha halisi kutoka 2020, "alisema.
Madowo alijiunga na CNN Mei 2021, miezi michache baada ya kuondoka BBC.
Mnamo Julai 2021, aliinuliwa hadhi kutoka kwa mwandishi wa CNN jijini Nairobi hadi mwanahabari wa kimataifa wa shirika hilo.
Aliingia kwenye mitandao ya kijamii ili kutoa taarifa kuhusu hali yake mpya ya kazi.
Kabla ya kufanya kazi katika CNN, Madowo aliwahi kuwa Mwandishi wa BBC wa Amerika Kaskazini katika Washington.
Pia alikuwa mtangazaji maarufu wa kipindi cha BBC World News America ambacho kinaonyeshwa kote ulimwenguni na kwenye vituo vya PBS kote Marekani.
Madowo mzaliwa wa Kenya alianza kazi yake ya utangazaji katika KTN akiwa na umri wa miaka 20.
Wakati akitangaza kazi yake ya wakati huo katika CNN, Madowo alionyesha furaha yake kufanya kazi nyumbani tena.
"Madowo alisema alifurahia kuripoti kutoka Marekani na duniani kote, lakini ni fursa nzuri sana kurejea Afrika katika wakati mgumu kama huu nchini Kenya na kote barani."
"Kwa muda mrefu nimefurahia utangazaji wa kushinda tuzo wa CNN International, na nina heshima kwa kujiunga na timu hiyo yenye vipaji.
Ninatazamia kushiriki wigo kamili wa maisha katika mojawapo ya sehemu zenye nguvu zaidi za dunia na watazamaji wa kimataifa wa CNN, " alisema.
Madowo hapo awali aliwahi kuwa Mhariri wa Biashara wa BBC Afrika.