logo

NOW ON AIR

Listen in Live

King Kaka aeleza alivyokabiliana na ugonjwa na sababu za kuficha familia, marafiki na mashabiki ukweli kuhusu afya yake

Bi Owiti alifichua kwamba kwa wakati mmoja alipatwa na hofu nyingi alipoamka na kuona mumewe akiwa amesimama mbele ya kioo akilia huku akieleza jinsi anapenda familia yake. Tukio hilo lilimfanya akimbie kwa jirani yake mhubiri na akamsihi aende akaombee mumewe.

image
na SAMUEL MAINA

Burudani03 November 2021 - 06:00

Muhtasari


  • •Rapa huyo alieleza kwamba aliamua kuficha mkewe na mama yake ukweli mwingi kuhusu afya yake kwa kuwa hakutaka wapatwe na wasiwasi.
  • •Kaka alisema kuwa ugonjwa ulipoendelea kukithiri alipoteza uzito mwingi wa mwili, midomo yake ikawa nyekundu zaidi, ngozi yake ikawa nyororo kuliko kawaida kati ya dalili zingine za kuhofisha ambazo hakutaka mashabiki wake wajue.
  • •Nana Owiti alisema kuwa kwa upande wake alishindwa kustahimili pekee yake kutazama mume wake akiumia na akaomba usaidizi wa marafiki wake ili aweze kukabiliana na yale alikuwa anapitia.

Kwa kipindi cha zaidi miezi mitatu ambacho mwanamuziki Kennedy Ombima almaarufu kama King Kaka alikuwa anaugua mashabiki wake walikaa gizani kuhusu kilichokuwa kinaendelea maishani mwa nyota wao.

King Kaka hakuficha tu mashabiki wake pekee mbali pia familia yake pamoja na marafiki wake wengi wa karibu. Alichagua kuteseka pekee yake katika ukimya.

Alipokuwa kwenye mazungumzo na mke wake Nana Owiti katika mtandao wa Youtube, rapa huyo alieleza kwamba aliamua kuficha mkewe na mama yake ukweli mwingi kuhusu afya yake kwa kuwa hakutaka wapatwe na wasiwasi.

"Mimi binafsi huona kama kwamba nitaweza kusuluhisha shida zangu wiki ijayo ama kesho. Nahitaji kulinda mke wangu kwa kukosa kumwambia ukweli wangu. Kuna uongo mzuri kama wakati nimeenda kupimwa uzani wa mwili nikata niko na kilo 68 kisha nikwambie (Nana) niko na kilo 74. Huo ni uongo mzuri kwa sababu sitaki Nana alale akiwa na wasiwasi. Uongo huo umetoka mahali pazuri kwa kuwa nampenda. Hautaki mtu unapenda alale na wasiwasi. Sikutaka pia mama apatwe na wasiwasi. Mama akiuliza naendelea aje kwa simu nasikika nikiwa na afya" King Kaka alieleza.

Nana Owiti alifichua kwamba kando na kupungua  sana kwa uzito wa mwili, mumewe pia alimficha kuhusu kikohozi cha kutisha ambacho alikuwa akitoa na pamoja na matokeo ya vipimo vya X-ray.

Bi Owiti alisema kuwa alishtuka sana siku moja alipoona kikohozi ambacho mumewe alikuwa amemficha kwa muda.

"Alikuwa anaficha bilauri fulani. Siku moja nikasema niangalie ni nini alikuwa anatematema. Alikuwa anatupa haraka sana kila asubuhi alipoamka. Nikasema niamke haraka asubuhi moja nijue ni nini kilichokuwa kinaendelea. Niliona kitu cha kushtua zaidi. Niliona akitema kikohozi kikubwa chenye rangi ya kijani na manjano. Siku moja angejaza bilauri ya nusu lita. Pia alikuwa na nyingine kwa gari" Nana Owiti alisimulia.

Wapenzi hao wawili walifichua kwamba kwa wakati huo walikuwa wamekata tamaa kiasi cha kwamba waliomba maradhi ambayo Kaka alikuwa anaugua yawe ni TB kuona kuwa vipimo vya daktari havikuwa vinabaini ugonjwa aliokuwa anaugua.

Kaka alisema kuwa ugonjwa ulipoendelea kukithiri alipoteza uzito mwingi wa mwili, midomo yake ikawa nyekundu zaidi, ngozi yake ikawa nyororo kuliko kawaida kati ya dalili zingine za kuhofisha ambazo hakutaka mashabiki wake wajue.

"Nilikuwa navaa koti yenye kofia kila nilipokuwa napiga picha. Nilikuwa nakaa takriban wiki tatu kama sijapakia picha kwa mtandao wa Instagram. Kila wakati nilikuwa napakia picha nikiwa nimevalia koti yenye kofia, barakoa huku nikiwa nimetazama chini. Midomo yangu ilikuwa nyekundu zaidi na nilikuwa nimefura. Kwa wakati huo tulikuwa tunajaribu tu kutafuta suluhu" Kaka alisema.

Baba huyo wa watoto watatu alisema kuwa kwa wakati huo ambapo alikuwa anaugua hakuwa anapatana na marafiki wake. Alisema kwamba alikuwa anawaepuka kila wakati ili wasione yaliyokuwa yamempata.

Kaka alieleza kwamba hakutaka kubebesha watu mzigo wa matatizo yake ila alitaka kuyasuluhisha mwenyewe.

"Kila ninapokabiliwa na shida huwa nataka niisuluhishe kwanza. Huwa sipendi kubebesha watu mzigo. Mimi ndiye mtu ambaye watu huletea mashida zao, huwa siendi kwao. Wakati huo nilipimwa na kila kitu nilichokuwa nacho na ilikuwa inabidi niende kwa watu ila sikutaka kuacha mwenendo wangu. Kutoambia watu ni tabia yangu" Kaka alisema.

Nana Owiti alisema kuwa kwa upande wake alishindwa kustahimili pekee yake kutazama mume wake akiumia na akaomba usaidizi wa marafiki wake ili aweze kukabiliana na yale alikuwa anapitia.

Bi Owiti alifichua kwamba kwa wakati mmoja alipatwa na hofu nyingi alipoamka na kuona mumewe akiwa amesimama mbele ya kioo akilia huku akieleza jinsi anapenda familia yake. Tukio hilo lilimfanya akimbie kwa jirani yake mhubiri na akamsihi aende akaombee mumewe.

"Walikuja wahubiri wanne wakiwa wamebeba mafuta ya upako wakamuombea na kwa namna kukawa na utulivu. Tukio hilo lilikuwa la kuhofisha lakini" Nana Owiti alisema.

Kwa neema zake Mola, King Kaka ameendelea kupata nafuu na kwa sasa hata amerejea shughuli zake za kawaida ikiwemo kutumbuiza watu katika tamasha.,


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved