"Tulikata tamaa kiasi cha kwamba tuliomba iwe ugonjwa fulani" King Kaka afunguka zaidi kuhusu ugonjwa uliomwathiri miezi 3

Muhtasari

•King Kaka amefichua kwamba matatizo yake ya afya yalianza siku chache tu baada ya kutoka kwa likizo ambayo alikuwa ameenda na familia yake katika eneo la Pwani.

•Ugonjwa ulipoendelea kukithiri hisia yake ya ladha ilipotea, ngozi yake ikawa nyororo zaidi, akaanza kukohoa, uzani wa mwili wake ukaanza kupungua, midomo yake ikawa nyekundu zaidi kati ya dalili zingine za kuhofisha.

•Baba huyo wa watoto watatu alifichua kwamba kwa wakati mmoja alikuwa ameshindwa kupumua kabisa.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Staa wa nyimbo za kufoka Kennedy Ombima almaarufu King Kaka amefunguka kuhusu ugonjwa uliokuwa umemwathiri kwa kipindi cha zaidi ya miezi mitatu.

Akiwa kwenye mahojiano na mke wake Nana Owiti katika mtandao wa YouTube, King Kaka amefichua kwamba matatizo yake ya afya yalianza siku chache tu baada ya kutoka kwa likizo ambayo alikuwa ameenda na familia yake katika eneo la Pwani.

Rapa huyo amesema kwamba alfajiri moja alirauka huku akiwa na maumivu tele kwenye koo  na akaamua kutafuta matibabu hospitalini.

"Tulikuwa tumeenda likizo Mombasa pamoja na familia. Watoto walikuwa wamekaa kwa nyumba sana kwa sababu ya janga la la Corona, tulihisi ni vyema wasafiri. Tulienda Pwani kujibaba. Tuliporudi, baada ya siku chache niliamka siku moja nikiumwa  na koo hadi sikuweza kumeza mate. Tulikimbia kwa hospitali iliyokuwa karibu na nikaambiwa kwa sababu singeweza kumeza dawa nikapewa antibiotics. Sijui kilichofanyika wakati huo ila nilianza kupata nafuu. Nilipatiwa  antibiotics za siku tano, nilikuwa nadungwa nne kila siku. Ningeenda hospitali kudungwa. Ikaisha lakini baada ya wiki tatu ikarudi" King Kaka alisimulia.

Wakati ugonjwa ule ulirejea mwanamuziki huyo alianza kuomba ushauri kutoka kwa marafiki wake ambao ni daktari.

Ugonjwa ulipoendelea kukithiri hisia yake ya ladha ilipotea, ngozi yake ikawa nyororo zaidi, akaanza kukohoa, uzani wa mwili wake ukaanza kupungua, midomo yake ikawa nyekundu zaidi kati ya dalili zingine za kuhofisha.

"Nilikuwa navaa suruali naona kwamba hainitoshei nachukua nyingine. Nilikohoa kwa kipindi cha wiki mbili hivi. Nilianza kutokwa na jasho usiku. Nilikuwa napigia marafiki wangu madaktari wakanipa ushauri" Kaka alisema.

Baada ya kuona kuwa uzito wa mwili wake ulikuwa unaendelea kupungua kila siku, daktari alipendekeza aanze kufanyiwa vipimo mbalimbali ili kubaini ugonjwa uliokuwa umemwathiri.

Kati ya vipimo ambavyo alifanyiwa ni pamoja na vipimo vya kifua kikuu, Ukimwi, Saratani, ugonjwa wa sukari kati ya maradhi mengine.

"Kulingana na uchunguzi wetu wa google tulikuwa tumeona kuwa mtu akipoteza kilo 10 na zaidi huenda anaugua Ukimwi, Saratani, Ugonjwa wa sukari, TB. Tulisema acha tuandike magonjwa hayo tuanze kuyapima tukitoa. Tulifanya vipimo vya Ukimwi ikapatikana sina, tukapima ugonjwa wa sukari, daktari akapendekeza tupime TB. Kwa wakati mmoja tulikuwa tumekata tamaa kwa sababu ugonjwa haukuwa unapatikana. Nilifanyiwa X-Ray ya kifua ikasemekana kuwa kuna dalili za Pneumonia. Tulikuwa tumekosa matumaini ikafika  mahali tukaanza kuomba iwe ugonjwa fulani ili ijulikane ugonjwa ambao utatibiwa" Alisema.

Baba huyo wa watoto watatu alifichua kwamba kwa wakati mmoja alikuwa ameshindwa kupumua kabisa.

Alisema kwamba ingawa alikuwa na hofu, ilimchukua muda kukubali kuwa hali yake ilikuwa mbaya.

"Kuna siku nilienda kwa kioo na nilipoangalia nikajiuliza ni nani huyo. Hata singeweza kujitambua. Nilijawa na hofu. Nilihofia mke wangu, watoto na mama yangu" Alisema.

Mwanamuziki huyo alifichua kwamba uzito wa mwili wake ulikuwa umepungua na takriban kilo 33. Alisema kuwa kwa kawaida alikuwa na  takriban kilo 85. 

Kwa neema zake Mola, King Kaka ameendelea kupata nafuu na kwa sasa hata amerejea shughuli zake za kawaida ikiwemo kutumbuiza watu katika tamasha.,