Mwanasosholaiti maarufu wa Kenya Vera Sidika amepuuzilia mbali madai kwamba aligura Ukristo na kubadili dini kuwa Muislamu.
Kwa muda, kumekuwa na ripoti kwamba mama huyo wa watoto wawili alibadili dini mwanzoni mwa uhusiano wake na Brown Mauzo.
Katika mahojiano ya hivi majuzi na Nairobi News hata hivyo, alikana kujiunga na Uislamu na kuweka wazi kuwa yeye bado ni Mkristo.
"Mimi ni Mkristo na yeyote anayeeneza madai ya uwongo kwamba nimebadili dini anapaswa kuacha kueneza uwongo," Vera Sidika alisema.
Aliendelea kusisitiza kuhusu hamu yake ya kurudi kanisani, mahali ambapo ameepuka kwa muda mrefu kutokana na jinsi anavyoangaziwa na watu wengi.
“Nimeeleza waziwazi hamu yangu ya kurejea kanisani. Sababu ambayo sijahudhuria kanisa ni kwa sababu ya umakini ninaovutia kama mtu maarufu na ukaguzi ninaokumbana nao kwa sababu ya hadhi yangu ya mtu mashuhuri," alisema.
Katika mahojiano ya awali, mume wa zamani wa mwanasosholaiti huyo Brown Mauzo alidai kuwa mama huyo wa watoto wake wawili alikuwa ameonyesha nia ya kugeuza dini kuwa Uislamu ili kuwa sawa naye.
Mwimbaji huyo mzaliwa wa Pwani alidai kuwa Vera alikuwa amechukua hata jina la Kiislamu ‘Zara’.
“Siku moja alinipigia simu na kueleza nia yake ya kubadili dini na kuwa Mwislamu, akisema alitaka tuwe wanandoa Waislamu. Hii ilikuwa ni dhabihu muhimu aliyokuwa anatoa kwa ajili ya uhusiano wetu na nikakubali,” Mauzo alisema.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Vera alidai kwamba mwaka huu wa 2024 angetaka kuboresha hata zaidi uhusiano wake na Mungu.
Sidika kupitia instastory zake, alisema kwamba angependa kuanza kuhudhuria ibada kanisani katika kipindi cha mwaka huu, akisema kwamba hiyo ndio njia pekee ya kuimarisha zaidi uhusiano wake na Muumba wake.
Kwa namna hiyo, Sidika aliwaomba mashabiki wake katika mtandao huo kumpa ushauri wa ni kanisa lipi zuri la kufanya mahudhurio ya ibada, akisema kwamba licha ya kuwa na uhusiano mzuri na Mungu, kwa muda mrefu sasa hajawai tia guu lake katika malango ya kanisa.
Mama huyo wa watoto wawili alisema kwamba aliwahi jaribu kufanya hivyo kwa wakati mmoja lakini akapata kila mtu macho yanamtoka pima pindi tu wanapomuona kanisani, jambo lililomchochea kujivuta nyuma katika suala zima la kwenda kanisani.
“Mwaka huu wa 2024 ninataka kujenga uhusiano mwema na Mungu, sijawahi kuenda kanisani kwa muda sasa, mimi ni muumini, namuomba Mungu na kufanya upande wangu kama Mkristo. Lakini inniwia vigumu kwenda kanisani. Watu wananiangalia sana. Kunaye mmoja wenu ambaye anajua kanisa zuri ambalo sitoweza kusumbuliwa na kuangaliwa, tafadhali pendekeza moja,” Vera Sidika aliomba.
Lakini pia alisisitiza kwamba asingependa kupendekezewa kanisa katika sehemu yoyote ile akisisitiza kwamba angependa kuhudhuria kanisa katika maeneo ya Kifahari ya Karen.
“Ikiwezekana iwe Karen,” Sidika aliongeza.