Huku maandalizi ya hafla ya mazishi ya mwanariadha Kelvin Kiptum yakiendelea kushika kasi katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, babake kijana huyo aliyefariki wiki jana amefichua kuwa ombi lake kuu ni kuona mwanawe wa pekee akizikwa kando na nyumba yake.
Hii ni baada ya serikali kujitosa katika mstari wa mbele kuharakisha ujenzi wa nyumba ya kifahari kwa ajili ya mwanariadha huyo mshikilizi wa rekodi katika mbio za marathon ambaye alifariki kutokana na ajali ya barabarani.
Serikali inajenga nyumba mbili kwa mpigo, moja ikiwa kwa ajili ya mjane wa Kiptum na nyingine ikiwa ya wazazi wake, na nyumba zote zitakuwa ndani ya boma moja zikiwa mkabala na kila moja.
Kiptum anatarajiwa kuzikwa wikendi ijayo nyumbani kwake katika kaunti ya Elgeyo Marakwet na kufikia sasa, ni mrundiko wa shughuli mbalimbali unaoendelea katika boma hilo kuhakikisha kwamba kila kitu kinakamilika kabla ya siku ya mazishi yake.
Hata hivyo, katika mahojaino, mjane Asenath alisema kwamba mpenziwe Kiptum alikuwa ameshapata shamba katika kaunti jirani ya Uasin Gishu ambapo walitarajia kuhamia baada ya kujenga nyumba ifikapo mwezi Juni mwaka huu.