logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Tutajenga kilabu ya usiku katika bustani ya Uhuru Park - Sakaja

Gavana huyo alitoa wito kwa umma haswa wakazi wa Nairobi kulinda mbuga hiyo na kuepuka vitendo vyovyote vya uharibifu.

image
na SAMUEL MAINA

Habari18 April 2024 - 13:00

Muhtasari


  • •"Kuna kilabu ya usiku ambayo itakuwa hapa. Tulikubaliana hiyo kupiga kelele kwa estate muache. Unaweza kuja hapa na kupiga kelele hadi ng'ombe warudi nyumbani," alisema.
  • •Gavana huyo alitoa wito kwa umma haswa wakazi wa Nairobi kulinda mbuga hiyo na kuepuka vitendo vyovyote vya uharibifu.
Waziri wa Ulinzi Aden Duale akiwa na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja wakati wa kukabidhi bustani ya Uhuru Park kwa Serikali ya Kaunti ya Nairobi mnamo Aprili 18, 2024.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ametangaza ujenzi wa kilabu ya usiku katika bustani ya Uhuru Park.

Sakaja alisema hii itawapa watu njia mbadala ya kufunguliwa kwa vilabu vya usiku katika uwanja huo.

"Kuna kilabu ya usiku ambayo itakuwa hapa. Tulikubaliana hiyo kupiga kelele kwa estate muache. Unaweza kuja hapa na kupiga kelele hadi ng'ombe warudi nyumbani," alisema.

"Hiyo ndiyo sehemu, sherehe mfanyie hapo."

Alisema miradi ya ziada katika bustani hiyo ambayo pia inajumuisha migahawa ya Waswahili na ya Kiafrika miongoni mwa mingine itajengwa chini ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPPs).

Maeneo mahsusi yatakapowekwa vifaa hivyo, alisema, tayari yametambuliwa na kuwahakikishia wale wanaopenda kuendesha biashara hizo miongoni mwa wengine katika hifadhi hiyo kuwa mchakato huo utakuwa wa uwazi.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hifadhi hiyo iliyotengenezwa na Wizara ya Ulinzi, Sakaja alisema hivi karibuni watafungua mchakato wa utoaji zabuni kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma na Uondoaji wa Mali (PPDA).

Wakati uo huo, gavana huyo alitoa wito kwa umma haswa wakazi wa Nairobi kulinda mbuga hiyo na kuepuka vitendo vyovyote vya uharibifu.

Aliwaambia wazingatie sheria za hifadhi ambazo ziko kwenye lango la kituo hicho.

Alibainisha kuwa shughuli zinazofanywa zilikuwa na gharama kubwa.

Waziri wa Ulinzi Aden Duale akiwa na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, maafisa wengine na maafisa wa usalama wakati wa kukabidhi bustani ya Uhuru Park kwa Serikali ya Kaunti ya Nairobi mnamo Aprili 18, 2024.

“Tujitolee katika kuitunza na kuiboresha hifadhi hii na mbuga nyinginezo kote jijini,” alisema huku akiwataka waliovamia kuhama mara moja.

"Kila aliyevamia hifadhi fanya mwenyewe tu ili tukija usiseme tumebomoa maana hatutoki mpaka tuirejeshe."

City Park, aliongeza, inatazamiwa kukabidhiwa kaunti kutoka kwa Huduma ya Misitu ya Kenya (KFS).

Mnamo Novemba 2022, Jumba la Jiji lilighairi leseni za vilabu vya usiku ambavyo vilikuwa vikifanya kazi katika maeneo ya makazi na kusema kuwa haitakuwa ikitoa vibali vya majengo kama hayo tena.

Sakaja alisema kuendelea mbele, leseni za vilabu vya usiku zitatolewa tu kwa majengo yanayofanya kazi ndani ya Wilaya ya Biashara ya Kati na mitaa iliyoainishwa ndani ya maeneo maalum ya makazi.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved