Mbunge Maalum Jackson Kosgei hatimaye ameeleza hisia na yale yote alipitia akiwa mikononi mwa waandamanaji katika majengo ya bunge siku ya Jumanne.
Kosgei ambaye ni babake mzazi wa mwanamuziki wa injili Emmy Kosgei aliingia bungeni baada ya kuteuliwa na chama tawala cha UDA.
Siku ya Jumanne wakati waandamanaji walivunja ukuta wa bunge na kuingia ndani mbunge huyo aliachwa na wenzake.
Mbunge huyo ambaye ni mlemavu wa miguu alikumbuka matukio ya Jumanne, Juni 25, wakati wa maandamano ya #OccupyParliament kupinga Muswada wa Fedha wa 2024.
Wabunge wengine walilazimika kukimbilia usalama wao wakati vijana wa Gen Z walipovunja ua na kuingia bungeni kwa nguvu licha ya vizuizi vya usalama vilivyokuwa vimewekwa.
Takriban watu 5 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati polisi walipowafyatulia risasi waandamanaji.
Baada ya kuchukuliwa na waandamanaji alisema vijana hao walmhakikishia kuwa hawatamdhuru.
"Licha ya ya kwamba ilikuwa katika hali ya hasira, walionyesha sura ya kibinadamu. Walipoingia walisema mzee tunakujua, ulikopiga kura, na tunakujua kama mtu mwema," alisimulia.
Katika video zilisosambaa mtandaoni, mbunge huyo alisindikizwa nje na kikundi kilichomuhakikishia usalama.
"Kwa hiyo walisema suala la wapi ulipiga kura na kadhalika sio hoja. 'tunataka kukusaidia kwa sababu kinachoweza kutokea hapa kinaweza kisiwe kizuri kwako," Kosgei alisema.