logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Marekani yasema Israel itaanza kusitisha vita kwa muda kwa saa nne kila siku huko Gaza

Biden alisema kutakuwa na "njia mbili za kibinadamu" zinazoruhusu watu kuondoka mapigano.

image
na Davis Ojiambo

Habari10 November 2023 - 06:11

Muhtasari


  • • Picha kwa mara nyingine tena zilionyesha maelfu ya Wapalestina wakikimbia kuelekea kusini kutoka mji huo na maeneo mengine ya kaskazini.

Israel itaanza kutekeleza usitishaji wa vita kwa saa nne kila siku katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza, msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Marekani John Kirby alisema.

Hata hivyo waziri wa ulinzi wa Israel alisisitiza kuwa "zitakuwa hatua za ndani na kubainisha kuwa "hazitazuia mapigano ya vita".

Rais Biden alisema kutakuwa na "njia mbili za kibinadamu" zinazoruhusu watu kuondoka katika maeneo ya mapigano.

Siku ya Alhamisi mapigano makali yaliripotiwa karibu na hospitali mbili kubwa katika Jiji la Gaza.

Wakati huo huo, picha kwa mara nyingine tena zilionyesha maelfu ya Wapalestina wakikimbia kuelekea kusini kutoka mji huo na maeneo mengine ya kaskazini.

Bw Biden pia alisema Marekani inajaribu kuongeza vifaa vya kibinadamu na usaidizi kwa Gaza.Alisema analenga lori 150 za msaada kwa siku kuingia katika eneo hilo.

Hata hivyo Umoja wa Mataifa ulisema kiasi cha misaada inayoingia Gaza ilikuwa inakidhi "sehemu" tu ya mahitaji ya watu na hali ya kibinadamu "haivumiliki".Mkutano wa mjini Paris hapo awali ulisikiliza maombi ya mara kwa mara ya kusitisha mapigano huko Gaza.

Israel imekuwa ikishambulia kwa mabomu Gaza kwa zaidi ya mwezi mmoja na ilianza mashambulizi makubwa ya ardhini takriban wiki mbili zilizopita kwa lengo la kuiangamiza Hamas, ambayo Marekani na mataifa mengine yenye nguvu ya Magharibi yanaona kuwa ni kundi la kigaidi.

Vita hivyo vilianza baada ya shambulio la kuvuka mpaka ambalo halijawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel na watu wenye silaha wa Hamas tarehe 7 Oktoba, ambapo watu 1,400 waliuawa na wengine 240 kuchukuliwa mateka.

Wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas imesema watu 10,800 wameuawa katika eneo hilo tangu wakati huo, huku milioni 1.5 wakikimbia makwao.

Bw Biden alisema Israel "inapambana na adui aliyejikita katika raia, jambo ambalo linawaweka Wapalestina wasio na hatia hatarini" lakini Israel ina "wajibu wa kutofautisha kati ya magaidi na raia na kufuata kikamilifu sheria za kimataifa".


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved