KAMPUNI ya kusambaza umeme nchini Kenya (KPLC) imeonya kuhusu kukatizwa kwa umeme katika maeneo kadhaa nchini siku ya Alhamisi, Julai 25.
Katika taarifa ya Jumatano jioni, kampuni hiyo ilisema kukatizwa kwa umeme kutatokana na ukarabati ambao utakuwa ukifanyiwa kwenye mitambo.
Walisema baadhi ya maeneo ya kaunti saba za Kenya yatakosa umeme kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi na moja jioni. Kaunti ambazo zitaathirika ni pamoja na Nakuru, Uasin Gishu, Kisii, Nyeri, Tharaka Nithi, Murang'a, na Kiambu.
Katika kaunti ya Nakuru, sehemu kadhaa za maeneo ya Naivasha Southlake, Kapkures na Ngamboo zitaathirika na kukatizwa kwa umeme kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi alasiri.
Baadhi ya sehemu za maeneo ya Kahoya na Bondeni katika kaunti ya Uasin Gishu zitaathirika na kukatizwa kwa umeme kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi alasiri.
Maeneo ya Boitangare na Nyamagwa katika kaunti ya Kisii yataathirika kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi alasiri.
Maeneo ya Ndunyo, na Guthuthi Tea Factory katika kaunti ya Uasin Gishu yataathirika kati ya saa tatu na saa kumi na moja jioni.
Katika kaunti ya Tharaka Nithi, maeneo ya Kaanwa na Kanjuki yataathirika kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi alasiri.
Sehemu za maeneo ya Murang'a na Sabasaba katika kaunti ya Murang'a pia zitaathirika kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Wakati huohuo, sehemu za miji ya Kiambu, Juja, na Kenyatta Road katika kaunti ya Kiambu pia zitaathirika.