logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Majonzi! afisa wa gereza la Kodiaga ajiua kwa risasi

Afisa huyo mwenye umri wa miaka 37 Fred Oganyo, anadaiwa kujipiga risasi Jumatano usiku.

image
na Davis Ojiambo

Habari24 March 2022 - 07:10

Muhtasari


  • • Afisa wa magereza amejiua kwa kujipiga risasi katika Gereza la Kisumu Maximum almaarufu Kodiaga Jumatano usiku.
  • • Kabla ya kuondoka, inasemekana kwamba afisa huyo alikuwa amewaambia watoto kwamba akifa, mali yake inapaswa kuwekwa vyema.
  • • Mmoja wa watoto, mtoto wake wa kwanza amefanya mtihani wa KCPE na anasubiri matokeo wiki ijayo. 
Fred Oganyo, afisa wa magereza katika gereza la Kodiaga GK ambaye anadaiwa kujipiga risasi na kujiua Jumatano usiku.

Afisa wa magereza amejiua kwa kujipiga risasi katika Gereza la Kisumu Maximum almaarufu Kodiaga Jumatano usiku. Tukio hilo lilitokea mwendo wa saa tatu unusu usiku wa Jumatano. Afisa huyo wa kiume anadaiwa kujipiga risasi kichwani kwenye kizuizi kikuu cha gereza hilo. 

Maafisa wa upelelezi kutoka idara ya DCI eneo la Maseno kaunti ya Kisumu tayari wameanzisha uchunguzi kubaini kilichochochea kifo cha afisa huyo.

Afisa huyo mwenye umri wa miaka 37 aliyetambulika kama Fred Oganyo, anadaiwa kujipiga risasi akiwa kazini Jumatano usiku.

Kulingana na mke wa afisa huyo Mercy Onyango, baba huyo wa watoto watatu alikuwa amepewa kazi za uangalizi katika lango kuu la gereza hilo tukio hilo la kusikitisha liliporipotiwa.

Alikuwa na wenzake wawili ambao walikuwa wamepewa majukumu ya kuchunga lango kuu la kituo kulingana na mkewe.

“Nilimkuta kwenye lango kuu, akiwa na wenzake wawili niliporudi kutoka kazini. Ilikuwa karibu saa mbili unusu mchana," alisema.

Waliongea na hata akaomba pesa kwa marehemu ili akanunue chakula. Alipofika nyumbani, kulikuwa na fujo.

Vitu vya nyumbani vilikuwa vimetawanywa katika chumba kimoja ambacho familia iliishi na watoto wao watatu, wasichana wawili na mvulana.

Kabla ya kuondoka, inasemekana kwamba afisa huyo alikuwa amewaambia watoto kwamba akifa, mali yake inapaswa kuwekwa vyema.

“Alikuwa amelewa. Sielewi kwa nini alipewa bunduki katika hali hiyo. Aliondoka nyumbani kwa fujo," aliambia Star kwenye simu. 

Mmoja wa watoto, mtoto wake wa kwanza amefanya mtihani wa KCPE na anasubiri matokeo wiki ijayo. 

“Hatukugombana. Sifahamu tofauti zozote ambazo anaweza kuwa nazo na mtu yeyote mahali pake pa kazi," alisema mkewe. 

Alisema mumewe alikuwa na jeraha la risasi kifuani mwake. Mwili wake ulipelekwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga mjini Kisumu. 

Kamanda wa polisi kaunti ya Kisumu, Alphonse Peter alisema matokeo ya awali yanaonyesha afisa huyo alikwa na msongo wa mawazo.

 "Alikuwa na mambo ya kifamilia ambayo hayajatatuliwa. Tumekuwa tukiwahimiza maafisa kujadili matatizo haya na wasiri wao badala ya kujiua,” alisema. 

"Hatuwezi kuthibitisha kwa uhakika kama alikuwa amelewa lakini ukweli ni kwamba, alisongwa na mawazo," alisema. 

Mkuu wa polisi wa kaunti alibainisha kuwa ripoti kamili itatolewa mara tu wapelelezi watakapokamilisha uchunguzi wao. 

Marehemu aliajiriwa katika huduma hiyo mwaka wa 2007 kulingana na mkewe.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved