29 wajeruhiwa katika mlipuko wa kiwanda cha gesi Nairobi

Msemaji wa serikali Isaac Mwaura alisema mitungi ya gesi ilikuwa ikijazwa tena moto ulipozuka kabla ya saa sita usiku Alhamisi.

Muhtasari

• Mashahidi waliambia vyombo vya habari kuwa walihisi tetemeko mara baada ya mlipuko huo.

Wazima moto wakiwa katika eneo la mlipuko katika ghala la kujaza mitungi ya gesi katika mtaa wa Mradi, wilaya ya Embakasi, Nairobi.
Wazima moto wakiwa katika eneo la mlipuko katika ghala la kujaza mitungi ya gesi katika mtaa wa Mradi, wilaya ya Embakasi, Nairobi.
Image: BBC

Takriban watu 29 wamejeruhiwa na wengine wengi wanahofiwa kujeruhiwa au kuuawa baada ya mlipuko katika kiwanda cha gesi kusini-mashariki mwa Nairobi, Kenya.

Video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha moto mkubwa ukiwaka karibu na majengo ya ghorofa katika eneo la Embakasi.

Msemaji wa serikali alisema mitungi ya gesi ilikuwa ikijazwa tena moto ulipozuka kabla ya saa sita usiku Alhamisi.

Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana, Isaac Mwaura alisema.

Wazima moto na wahudumu wa dharura wako katika eneo ambalo kampuni ya Kentainers Company Ltd ipo, kulingana na Bw Mwaura.

Aliongeza: "Jengo la kampuni hiyo limeharibiwa vibaya.

"Wananchi wanashauriwa kuepuka eneo hilo kwani shughuli za uokoaji zinaendelea ikiwa ni pamoja na vyombo vya moto kupelekwa eneo hilo."

Mashahidi waliambia vyombo vya habari kuwa walihisi tetemeko mara baada ya mlipuko huo.

Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema kwenye mitandao ya kijamii wafanyakazi wamekuwa "wakipambana na moto" na kusema kuwa watu 29 wamepelekwa hospitalini wakiwa na majeraha.

Moto huo unaripotiwa kuenea katika majengo kadhaa ya ghorofa, na kusababisha hofu kwamba idadi ya waliojeruhiwa inaweza kuongezeka zaidi.