Hakuna sheria nchini Kenya inayoharamisha mtu kuwa shoga - Seneta Edwin Sifuna (video)

" Nchi hii, ubakaji wa kisheria unaitwa ndoa ya mapema," Sifuna alisema.

Muhtasari

• Seneta huyo aliweka wazi kwamba kilichopo ni kanuni ya adhabu inayoweka adhabu ya kufanya ngono ambayo ni kinyume na utaratibu wa asili.

Mgombea wa useneta wa Nairobi Edwin Sifuna wakati wa kibali Kasarani.
Mgombea wa useneta wa Nairobi Edwin Sifuna wakati wa kibali Kasarani.

Seneta wa Nairobi ambaye pia ni katibu wa kitaifa wa chama cha upinzani cha ODM, Edwin Sifuna amezua utata miongoni mwa Wakenya baada ya kudai kwamba kufikia sasa hakuna sheria nchini Kenya inayoharamisha mtu yeyote kuchagua kuwa shoga au la.

Akizungumza katika runinga ya Citizen, seneta huyo aliweka wazi kwamba kilichopo ni kanuni ya adhabu inayoweka adhabu ya kufanya ngono ambayo ni kinyume na utaratibu wa asili, ikiwa ni pamoja na kati ya mwanamume na mwanamke.

“Hakuna sheria nchini Kenya dhidi ya kuwa mashoga. Sheria hiyo haipo; unaiunda tu. Kanuni ya adhabu inaweka adhabu ya kufanya ngono kinyume na utaratibu wa asili, ikiwa ni pamoja na kati ya mwanamume na mwanamke. Nchi hii, ubakaji wa kisheria unaitwa ndoa ya mapema," Sifuna alisema.

Tamko hili ambalo wengi wa Wakenya wamelichukua nje ya muktadha linakuja wakati ambapo viongozi wengi wakiongozwa na mke wa naibu rais, Mama Dorcas Gachagua ako katika mstari wa mbele kupinga ujio wa vitendo na visa vya ushoga, maarufu kama LGBTQ.