Wakaazi wa mtaa wa Kikopey katika eneo la Gilgil mnamo siku ya Alhamisi walikuwa wakijaribu kukubaliana na shambulio la kushangaza ambapo mwanamume mwenye umri wa miaka 30 alimuua mkewe waliyeachana naye kwa kumkata koromeo.
Wakati wa kisa hicho kilichotokea katika mojawapo ya nyumba za kulala wageni, mwanamume huyo aliyekuwa amesafiri kutoka mji wa Eldoret alijidunga kisu kifuani na tumboni katika jaribio linaloshukiwa la kujitoa uhai.
Mshukiwa, ambaye anapigania maisha yake hospitalini, alikuwa amesafiri kwa takriban kilomita 200 kumshawishi mwanamke huyo wa miaka 23 kurejea nyumbani, kabla ya kumgeuka.
Sakina Mohammed kutoka Lifebloom International Services alisema wanandoa hao walitengana mwaka jana, na kumlazimu mama huyo wa mtoto mmoja kuhamia Gilgil.
Mwanamume huyo alikuwa amemtembelea mara kadhaa akijaribu kumshawishi arudi nyumbani lakini mwanamke huyo alikuwa na msimamo mkali hadi Jumatano jioni shambulio hilo lilipotokea.
"Mwanamume huyo alimvuta katika moja ya nyumba za kulala wageni ili wazungumze na kutatua tofauti zao lakini alimgeuka na kumkata koo na tumbo," Mohammed alisema.
Mwanaharakati huyo, ambaye anahusika katika kusaidia watoto na wanawake walionyanyaswa, alisema kuwa wafanyakazi waliosikia kilio cha mwanamke huyo waliwapigia simu polisi ambao walifika na kumkuta mwanaume huyo akivuja damu nyingi.
Naibu Kamishna wa Kaunti ya Gilgil Willy Cheboi alithibitisha kisa hicho na kuongeza kuwa mshukiwa amepelekwa Nakuru kwa matibabu maalum.
"Polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo huku wakisubiri mshukiwa apate nafuu ili arekodi taarifa na kutoa mwanga zaidi kuhusu tukio hili," alisema.
Huku hayo yakijiri, mwanamume aliyemnyunyizia mkewe maji ya moto na baadaye kumdunga kisu tumboni kufuatia mzozo wa kinyumbani Naivasha ametiwa mbaroni.
Afisa huyo wa zamani wa polisi ambaye kwa sasa anafanya kazi na serikali ya Nakuru kama afisa wa utekelezaji alikamatwa katika mji wa Naivasha baada ya wiki moja ya kujificha kutoka kwa polisi.
Wiki iliyopita, mwanamume huyo alidaiwa kuchemsha maji na kummwagia mkewe aliyekuwa amelala kabla ya kumchoma kisu na kuacha sehemu ya viungo vyake vya ndani vikining’inia.
Kulingana na John Kinuthia kutoka Kundi la Jinsia laNaivasha, kukamatwa kwa mshukiwa kulitimia kwa wakati kwani alimtishia mwathiriwa ambaye amelazwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha.
"Tunashukuru polisi kwa kuingia na kumkamata mshukiwa ambaye amekuwa akipiga kifua, akidai kuwa hangeweza kukamatwa na tunatumai mwathiriwa atapata haki," Kinuthia alisema.
Utafsiri: Samuel Maina