Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico anapigania maisha yake hospitalini baada ya kupigwa risasi katika mji mdogo kaskazini-mashariki mwa Bratislava.
Siku ya Jumatano jioni Waziri wa Ulinzi Robert Kalinak alisema Bw Fico amekuwa akifanyiwa upasuaji kwa zaidi ya saa tatu na kwamba hali yake ilikuwa "mbaya".
Wanasiasa wa Slovakia akiwemo rais wametaja tukio hilo kuwa "shambulio dhidi ya demokrasia".
Mtuhumiwa huyo anazuiliwa katika eneo la tukio lakini bado hajatambuliwa rasmi na mamlaka.
Shambulio hilo lilitokea mwendo wa saa 14:30 (12:30 GMT) huko Handlova, takriban kilomita 180 kutoka mji mkuu Bratislava, wakati Bw Fico akisalimiana na watu mbele ya kituo cha jumuiya ya kitamaduni ambapo mkutano wa serikali ulikuwa umefanyika.
Picha zilionyesha mwanamume akinyanyua bunduki na kumfyatulia risasi waziri mkuu mara tano kabla ya kukamatwa na walinzi huku maafisa wengine wa usalama wa Bw Fico wakimuingiza waziri mkuu kwenye gari lake.
Alisafirishwa kwa helikopta hadi katika hospitali iliyo karibu kabla ya kupelekwa hadi hospitali nyingine huko Banska Bystrica, mashariki mwa Handlova.
Baadaye siku ya Jumatano Naibu Waziri Mkuu wa Slovakia Tomas Taraba aliambia kipindi cha BBC cha Newshour kwamba anaamini kuwa hali ya Bw Fico hospitalini inaendelea kuwa nzuri.
"Nadhani mwishowe atapona," Bw Taraba alisema, na kuongeza: "Hayuko katika hali ya kutishia maisha kwa sasa."