In Summary

•Diana alifichua kuwa yeye pamoja na dada zake wadogo, Varl na Michelle  walilelewa na baba yao pekee yake baada yake kutengana na mama yao wakiwa na umri mdogo sana.

•Diana ameeleza kuwa Michelle alikuwa na hamu kubwa sana ya kujiunga na shule ya upili kwani ilimpa nafasi ya kutembelewa mara kwa mara na mama yake ambaye alikuwa ametengana na baba yao akiwa na miezi tisa tu

Diana Marua na dadake Michelle
Image: INSTAGRAM//DIANA MARUA

Diana Marua ambaye ni mkewe mwanamuziki Kevin Bahati amesimulia jinsi ndoto ya dadake mdogo Michelle ya kuona mamaye mara kwa mara iliangamia wiki tatu tu baada ya kujiunga na shule ya upili.

Kupitia akaunti yake ya YouTube Diana ameeleza kuwa Michelle alikuwa na hamu kubwa sana ya kujiunga na shule ya upili kwani ilimpa nafasi ya kutembelewa mara kwa mara na mama yake ambaye alikuwa ametengana na baba yao akiwa na miezi tisa tu.

Diana alifichua kuwa yeye pamoja na dada zake wadogo, Varl na Michelle  walilelewa na baba yao pekee yake baada yake kutengana na mama yao wakiwa na umri mdogo sana.

Kutengana kwa wazazi wao hakukuwapa nafasi nyingi za kumuona mama yao kwani kulikuwa na vizuizi vilivyowekwa kuhusu matembezi yake.

"Michelle alikuwa na furaha kuwa mama angekuwa anaenda kumuona shuleni na kupatana nafasi ya kujuana zaidi. Nakumbuka nikimwambia kuwa kweli huo ndio ulikuwa wakati mama angekuwa anaenda kumuona kwani ilikuwa ngumu sana kwake kuja kumuona Michelle kwani kulikuwa na vikwazo vya kinyumbani."  Diana alisimulia.

Diana alieleza kuwa ndoto ya dadake mdogo kupata nafasi ya kumuona mamaye mara kwa mara haikutimia kwani aliangamia kutokana na maradhi ya kisukari takriban wiki tatu tu baada yake kujiunga na shule ya upili ya Moi 

"Kipindi kifupi tu baada ya Michelle kujiunga na shule ya upili, sidhani hata alikuwa ametulia vizuri pale, takriban wiki mbili tatu hivi kwa bahati mbaya mamangu aliaga dunia .Alifariki baada ya kuugua kisukari kwa kipindi kifupi" Alisema Diana.

Alisema kuwa jukumu ngumu iliyokuwepo ilikuwa kumfahamisha dada yake Michelle kuwa hangeweza kumuona mamake kwani alikuwa ameaga.

"Ilikuwa ngumu sana kumwambia Michelle. Nakumbuka babangu alienda kumchukua shule na hata kabla wafike nyumbani baba alilazimika kumwambia kuwa mama hakuwepo tena. Dunia ya dadangu ilikuwa imeporomoka kwani huu ndio wakati alikuwa amesubiri kwa hamu. Alijua kuwa alikuwa amepata nafasi ya kujuana vizuri na mama kwani mamangu hakuwahi kuwepo kote maishani mwake. Huo ndio wakati dadangu alidhani kuwa angepata nafasi ya kuwa na mama yake" Diana alisema.

Tukio hilo lilimfanya Diana kufanya maamuzi dhabiti ya kuchukua nafasi ya mama katika maisha ya dada zake wadogo.

"Baada ya kushuhudia utupu niliopitia kwa kukosa kielelezo cha mama maishani mwangu nilijiambia kuwa ningefanya kila kitu ningeweza ili kuhakikisha kuwa nimewapa dada zangu kila kitu kizuri. Nilisema kuwa singeruhusu ifike wakati maishani mwao waseme kuwa wanaumia kwa kukosa nafasi ya mama. Wanaweza kusema kuwa hawajui mapenzi ya mama lakini nilisema kuwa ningejaribu kadri ya uwezo wangu ikiwezekana nijaze nafasi hiyo. Kweli siwezi kujaza nafai ambayo mama yangu angecheza maishani mwao lakini kwa kuwa hayupo nitafanya kila kitukuhakikisha wamefurahia" Alisema Diana

Kuashiria mapenzi aliyo nayo kwa dada zake, Diana alimzawadi dadake Michelle ambaye kwa sasa ana ujauzito.

View Comments