In Summary

•Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mwanamuziki huyo mwenye umri wa takriban miaka 40 amedai kuwa mwanaume hawezi kumfanya aamue kujitia kitanzi.

•Ingawa Nyota Ndogo hajatangaza wazi kutengana kwao, jumbe zake za hivi karibuni zimeashiria kuwa huenda madai hayo ni ya kweli.

•Miezi kadhaa iliyopita mwanamuziki huyo aliandika jumbe moja baada ya nyingine akimsihi mumewe kumrudia baada ya wao kukosana mwezi Aprili.

nyota ndogo

Mwanamuziki mashuhuri kutoka Pwani amepuuzilia mbali uvumi kuwa amejitoa uhai baada ya kukosana na mpenzi wake mzungu.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mwanamuziki huyo mwenye umri wa takriban miaka 40 amedai kuwa mwanaume hawezi kumfanya aamue kujitia kitanzi.

"Nimetoka kumpigia mama simu kabla hajaambiwa na majirani.. siwezi kujiua kwaajili ya mwanaume bwana" Aliandika Nyota Ndogo.

Nyota Ndogo alikuwa anajibu ujumbe uliokuwa umepakiwa kwenye mtandao wa Facebook  ukisema kuwa alikuwa amejitoa uhai baada ya kutengana na mumewe.

"Mwanamuziki Nyota Ndogo ajitoa uhai baada ya utengano wa kusikitisha na mumewe mzungu" Ujumbe huo ulisoma.

Hivi majuzi kumekuwa na tetesi kwamba mwanamuziki huyo ametengana na mumewe Henning Nielsen kutoka Denmark.

Ingawa Nyota Ndogo hajatangaza wazi kutengana kwao, jumbe zake za hivi karibuni zimeashiria kuwa huenda madai hayo ni ya kweli.

Mnamo Jumatatu msanii huyo aliandika ujumbe ambao uliashiria kuwa tayari amekubali kilichotokea na ako tayari kusonga mbele na maisha yake.

"Kuna muda unaweza kua unapigania kitu sana na kumbe sio chako tena. Kiachilie tu kiende. Tazama nilivyojawa na furaha kwa sababu nimekubali" Aliandika Nyota Ndogo chini ya picha aliyopakia Instagram akitabasamu.

Miezi kadhaa iliyopita mwanamuziki huyo aliandika jumbe moja baada ya nyingine akimsihi mumewe kumrudia baada ya wao kukosana mwezi Aprili.

Juhudi zake zilionekana kuzaa matunda kwani mnamo mwezi Juni mumewe alimtumia ujumbe akimwambia kuwa alikuwa anampeza.

View Comments