In Summary

•Hukumu dhidi ya R Kelly itatolewa mnamo Mei 4 mwaka ujao na huenda akapata kifungo kirefu zaidi ikiwemo uwezekano mkubwa wa kufungwa maisha.

Vybz Kartel, Lil Wayne, R Kelly
Image: HISANI

Siku ya Jumatatu wiki hii habari kuhusu mwanamuziki R Kelly kupatikana na hatia ya unyanyasaji wa kingono ziligonga vichwa vya habari kote duniani.

Staa huyo wa nyimbo aina ya Hiphop alipatikana na hatia ya kutumia hadhi yake ya kuwa nyota wa muziki wa R&B kuendesha mpango wa kuwadhulumu kingono wanawake na watoto kwa zaidi ya miongo miwili.

Hukumu dhidi ya R Kelly itatolewa mnamo Mei 4 mwaka ujao na huenda akapata kifungo kirefu zaidi ikiwemo uwezekano mkubwa wa kufungwa maisha.

Hata hivyo, Robert Kelly hatakuwa mwanamuziki wa kwanza mashuhuri kujipata akila kalenda. Kunao  wasanii kadhaa  mashuhuri ambao wamewahi kufungwa gerezani miaka ya hapo awali.

Hawa hapa baadhi yao na kwa nini walifungwa:-

Buju Banton

Image: HISANI

Mark Antony Myrie almaarufu kama Buju Banton alihudumu kifungo cha miaka 7 katika gereza moja nchini Marekani.

Mwanamuziki huyo wa nyimbo za reggea alipatiwa kifungo cha miaka 10 mnamo mwaka wa 2011 baada ya kupatikana na kosa la ulanguzi wa kokeni na umiliki wa bunduki haramu.

Hata hivyo mahakama ilitupilia mbali kesi iliyohusisha bunduki bandia na kupunguza kifungo chake na miaka miwili.

Mzaliwa huyo wa Jamaica aliachiliwa huru mwezi Desemba mwaka wa 2018.

Bobby Shmurda

Mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo za kufoka Ackquille Jean Pollard maarufu kama Bobby Shmurda aliachiliwa mwezi Februari mwakani baada ya kuhudumu kifungo cha miaka mitano gerezani nchini Marekani.

Shmurda alihukumiwa mwaka wa 2016 baada ya kukubali mashtaka ya umiliki wa silaha haramu.

Vybz Kartel

Image: HISANI

Adidja Azim Palmer maarufu kama Vybz Kartel alihukumiwa kifungo cha maisha mwaka wa 2014 baada ya kupatikana na kosa la mauaji.

Kartel alifungwa pamoja na wengine watatu kwa kosa la kuua mwanabiashara wa Jamaica aliyejulikana kama Clive 'Lizard' Williams.

Mwanamuziki huyo wa nyimbo aina ya dancehall atastahiki kupata msamaha baada ya kuhudumu miaka 33 gerezani.

Lil Wayne

Mwaka wa 2010 mwanamuziki wa nyimbo za kufoka Dwayne Michael Carter Jr maarufu kama Lil Wayne alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja baada ya kukubali mashtaka ya umulikaji wa silaha haramu.

Wayne hata hivyo aliachiliwa baada ya kuhudumu miezi minane katika gereza ya Rikers Island.

Tupac Shakur

Image: HISANI

Mwaka wa 1995 mwanamuziki Tupac Amaru Shakur alihudumu kifungo cha miezi tisa baada ya kupatikana na kosa la unyanyasaji wa kingono.

Marehemu Shakur alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka  1½ hadi 4½ katika gereza ya Clinton, Marekani ila akawachiliwa baada ya kuhudumu miezi tisa na kulipa dhamana ya dola milioni 1.4.

View Comments